Kocha Kagera ahaha kuziba pengo la Mbaraka

Thursday October 12 2017

 

By THOBIAS SEBASTIAN

Hatimaye kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amekiri kuwa pengo la aliyekuwa straika wao, Mbaraka Yusuf linawatesa wakati huu akijaribu kumtengeneza mbadala wake.

Mbaraka aliifungia Kagera Sugar mabao 12 msimu uliopita na kuisaidia kumaliza katika nafasi ya tatu ambayo ni ya juu zaidi kwao tangu walipoanza kushiriki Ligi Kuu miaka zaidi ya 12 iliyopita. Maxime alisema Mbaraka alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi chao na kukosekana kwake inaweza kuwa moja ya sababu ya timu kuanza vibaya msimu huu. Kagera imefunga bao moja pekee katika mechi tano ilizocheza msimu huu.

“Najaribu kutafuta mshambuliaji mwingine ambaye ataziba nafasi ya Mbaraka. Waliokuwepo bado hajawaweza kufikia kiwango hicho, hilo limekuwa kikwazo kwetu tangu tulipoanza ligi msimu huu,” alisema Maxime ambaye ni kocha bora wa msimu uliopita.