Kiungo yanga asaka vipaji Kagera

Muktasari:

Vijana waliojitokeza katika usaili huo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba wamegawanywa katika makundi tofauti kulingana na umri wao na baadhi yao kuchaguliwa kuendelea leo katika hatua inayofuata.

Bukoba. Kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Salvatory Edward ameanza kusaka wachezaji vijana watakaojiunga na kituo cha michezo cha Karume Sports Academy cha mjini Bukoba.

Vijana waliojitokeza katika usaili huo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba wamegawanywa katika makundi tofauti kulingana na umri wao na baadhi yao kuchaguliwa kuendelea leo katika hatua inayofuata.

Zoezi hilo limekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa vijana wakiwemo wanaoishi kwenye mazingira hatarishi wakiwa na kiu ya kukuza vipaji vyao kupitia kituo cha michezo cha Karume Sports  Academy.

Salvatory Edward alisema baadhi ya vijana walitawaliwa na woga, lakini anaamini baada ya wiki mmoja ya mchujo huo watapata vijana wengi.

Mkurugenzi wa Kituo hicho mchezaji wa zamani CDA-Dodoma, Seif Mkude alisema amefikia hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa vijana kuibuliwa na kuendelezwa kwa vipaji vyao katika soka kuanzia umri wa miaka 10 hadi 14 na kundi la umri wa kuanzia 14 hadi 19.