Kiberenge bado kidogo tu apete

Muktasari:

Kocha huyo, alisema amekoshwa na viwango vya baadhi ya wachezaji waliokuwa wakianzia benchi ndani ya timu hiyo, wakiwamo Geofrey Mwashiuya na Juma Mahadhi, lakini akimtaja Baruan Akilimali ‘Kiberenge’ kuwa ni mkali zaidi na akijiongeza kidogo tu atatisha.

YANGA ina kila dalili ya kushindwa kumaliza katika Mbili Bora ya Ligi Kuu Bara ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya misimu mitano, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera amejikuta akitabasamu kutokana na viwango vya nyota wake.

Kocha huyo, alisema amekoshwa na viwango vya baadhi ya wachezaji waliokuwa wakianzia benchi ndani ya timu hiyo, wakiwamo Geofrey Mwashiuya na Juma Mahadhi, lakini akimtaja Baruan Akilimali ‘Kiberenge’ kuwa ni mkali zaidi na akijiongeza kidogo tu atatisha.

Mwashiuya, Mahadhi na Akilimali walikuwa chaguo la pili chini ya utawala wa Kocha George Lwandamina, lakini Zahera amekuwa akiwapa nafasi katika mechi mfululizo.

Akizungumza na Mwanaspoti, kabla ya kutimka kwenda DR Congo, Kocha Zahera alisema wachezaji hao wana uwezo mkubwa wa kupekeleka mashambulizi kwa timu pinzani, huku akisisitiza ni jambo linalotakiwa kwa anayecheza nafasi za mawinga. “Wote hawa ni vijana wadogo wanaotakiwa wapewe akili mpya na kuachana na aina ya mchezo wa kitoto, wana nguvu na spidi, hivyo nikiwatengeneza upya, lazima watishe na hasa Akilimali,” alisema. “Kama umewafuatilia utawaona wana nguvu asili walizonazo, pia hata spidi yao ni nzuri, napenda mchezaji asiyeogop mabeki kama Mwashiuya na Akilimali.

Mahadhi ni muoga lakini ana spidi nzuri nitamtengeneza awe kama wenzake,” alisema Zahera.

Yanga inayojiandaa kuvaana na Mbao kesho Jumanne katika mechi yao ya kipro, ikiwa haijaonja ushindi katika Ligi Kuu Bara tangu walipoinyoosha Stand United kwa mabao 3-1 Machi 12, lakini ikicheza mechi 9 mfululizo za mashindano bila ushindi tangu ikimbiwe na Kocha Lwandamina aliyetimkia kwao Zambia mwezi uliopita.