Kennedy, Kaseke ni Simba

KOCHA Mfaransa, Pierre Lechantre ameondoka juzi mjini hapa ili kuanza safari ya kwenda kwao Ufaransa baada ya kushindwa kuafikiana na mabosi wa Simba juu ya mkataba mpya, lakini ameacha kazi maalumu kwa mabosi wa timu hiyo.

Lechantre hakukaa kwenye benchi wakati Simba ikicheza na Kakamega Homeboys kwenye pambano la nusu fainali kisha kuondoka mjini hapa usiku huo huo, lakini ameacha habari njema Msimbazi.

Lechantre ambaye amewahi kuwa kocha bora wa Afrika na Asia kwa nyakati tofauti, amewaambia mabosi wa Simba kama wanataka kuendelea kukiimarisha kikosi chao wawasajili nyota wawili wa maana kutoka Singida United.

Kocha huyo amesema kwa namna safu yao ya ulinzi inavyocheza sasa, ni dhahiri beki wa Singida United, Kennedy Juma anaweza kuingia kwenye kikosi cha kwanza na kufanya vizuri.

Mbali na Kennedy, kocha huyo amewaambia mabosi wa Simba waanze mazungumzo ya haraka na winga wa timu hiyo, Deus Kaseke kwani yuko kwenye kiwango bora kwa sasa.

Alisema Kaseke ni miongoni mwa mawinga wenye uwezo mkubwa zaidi nchini, akiwa na uwezo wa kumiliki mpira, kufungua timu pamoja na kutengeneza nafasi za kufunga.

Mbali na hilo, Kaseke pia amekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga, jambo ambalo litaongeza wigo wa washambuliaji wa timu yake kwani kwa sasa inamtegemea zaidi Shiza Kichuya kwenye winga zake.

Hata hivyo, Simba itakabiliwa na wakati mgumu wa kumpata Kaseke kwani tayari ana ofa nchini Afrika Kusini na huenda akaondoka mara tu baada ya kumalizika kwa michuano ya SportPesa Super Cup.

“Kennedy ni beki mzuri, amekuwa kwenye kiwango bora mpaka sasa na anaweza kuisaidia Simba. Nimewaambia viongozi wamchukue pamoja na yule winga anayevaa namba saba (Deus Kaseke).

“Huyu winga (Kaseke) anacheza vizuri, anamiliki mpira, anatengeneza nafasi na kufunga. Anaweza kutusaidia Simba kwa msimu ujao,” alisema Lechantre.

“Nimewaambia viongozi hata kama ninaondoka wachezaji hao ni vyema wakawasajili. Wameniambia gharama zao ni kubwa, lakini itakuwa vyema wakija,” alisema Lechantre saa chache kabla ya kwenda kwao Ufaransa.

ISHU YAKE

Simba bado imekuwa na kigugumizi cha moja kwa moja juu ya kuachana na Lechantre, lakini habari za ndani zinasema viongozi wa timu hiyo hawafurahishwi na namna timu yao inavyocheza.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Tryagain’ alisema watatoa ufafanuzi wa kile kinachoendelea baina yao na kocha huyo ambaye tayari ameondoka mjini hapa.

Pamoja na hayo, inaelezwa Lechantre aliamua kususa baada ya kuona mashabiki na viongozi wanamhusudu zaidi kocha msaidizi, Masoud Djuma hivyo kuamua kumwachia timu naye aonyeshe uwezo wake.

Imeelezwa pia Lechantre hana furaha kuendelea kufanya kazi wakati huu mkataba wake ukiwa umebakisha siku nane tu kabla ya kumalizika, huku habari za ndani zaidi zikieleza kuwa wanamtema kabisa kocha huyo.