Kakolanya ana akili yake

KIPA Beno Kakolanya amejitoa ndani ya Yanga ili kushinikiza kulipwa fedha zake za usajili zilizosalia, lakini kama hiyo haitoshi amepanga kuishtaki timu hiyo kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ili limsaidie apate chake.

Meneja wa mchezaji huyo, Seleman Haroub, amesema hawana tatizo na Yanga, ila wataipeleka TFF kuhakikisha mteja wake aweze kulipwa chake.

“Mwanzo tulikaa chini na wenzetu wa Yanga na kuweka makubaliano fulani na mikataba yote ipo, lakini bado hawakufanya vile tulivyokubaliana,” alisema.

Meneja huyo alisema walipanga kwenda TFF mapema ila wamesubiri kwanza msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya umalizike.

“Jumanne (kesho) nitapeleka barua TFF, kule ndio wataamua kipi kifanyike. Tulisubiri kwanza msimu wa sikukuu umalizike,” alisema.