Kaheza akitua tu, Okwi, Bocco wajipange aisee

Muktasari:

  • Kaheza alisema ana uhakika akitua Simba lazima aingie kikosi cha kwanza kwa vile ana uwezo mkubwa wa kuhimili ushindani licha ya ukubwa wa majina ya washambuliaji hao wakongwe waliofunga jumla ya mabao 34 kwa pamoja katika Ligi Kuu msimu huu.

WAKATI akiendelea kutajwa kuwa tu mbioni kutua Msimbazi, straika wa Majimaji Marcel Boniventure Kaheza, amefunguka na kudai kuwa hana hofu kabisa na kasi ya Emmanuel Okwi na John Bocco na kama kweli atatua Simba jamaa wajipange.

Kaheza alisema ana uhakika akitua Simba lazima aingie kikosi cha kwanza kwa vile ana uwezo mkubwa wa kuhimili ushindani licha ya ukubwa wa majina ya washambuliaji hao wakongwe waliofunga jumla ya mabao 34 kwa pamoja katika Ligi Kuu msimu huu.

Straika huyo mwenye mabao 13 hadi sasa, anahusishwa kujiunga na Simba na amethibitisha kufanya mazungumzo na mabosi wa Msimbazi, huku akisisitiza yupo tayari kuliamsha sambamba na akina Okwi.

“Sina wasiwasi ya kukosa namba licha ya kuwapo kwa kina Bocco (John) au Okwi(Emmanuel), naamini kiwango changu ni cha juu na nitapata nafasi tena kikosi cha kwanza,” alisema Kaheza.

Kuhusu hatma ya timu yake kushuka daraja, Kaheza alisema bado hawajakata tamaa hadi mechi yao ya mwisho na kwamba itategemeana na matokeo.