Juma Kaseja apewa ubosi Kagera Sugar

Muktasari:

  • Kaseja ambaye anakubalika zaidi na mabosi wa Kagera kutokana na kujitolea kwake ndani ya kikosi na wanamtaja kuwa ndiyo siri ya mafanikio kwenye timu ndani ya kipindi cha msimu uliopita mpaka wakamaliza nafasi ya tatu.

Mlinda mlango mkongwe kwenye Ligi Kuu Bara, Juma Kaseja amepewa ubosi ndani ya kikosi chake cha Kagera Sugar mbali na kukaa golini, atawaongoza walinda mlango wenzake kama kocha wa makipa.

Kaseja ambaye anakubalika zaidi na mabosi wa Kagera kutokana na kujitolea kwake ndani ya kikosi na wanamtaja kuwa ndiyo siri ya mafanikio kwenye timu ndani ya kipindi cha msimu uliopita mpaka wakamaliza nafasi ya tatu.

Amepewa jukumu hilo na atawaongoza makipa waliosajiliwa na Kagera msimu huu, Said Kipao kutoka JKT Ruvu na Ramadhani Chalambanda aliyeidakia Madini msimu uliopita.

Menaja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein ameliambia Mwanaspoti: "Kaseja amejenga uaminifu mkubwa ndani ya timu. Amekuwa chachu ya mafanikio katika timu na anautumia vizuri uzoefu wake katika kuwaongoza vijana."

Uongozi huo umempa majukumu Kaseja ambaye amecheza ligi kuu kwa misimu isiyopungua 15 na alizichezea klabu za Simba, Yanga, Moro United na Mtibwa Sugar kwa nyakati tofauti.