JKT wamfanyia pati Simbu

ASIKWAMBIE mtu, ushindi una raha zake bwana,  kwani mwanariadha Alphonce Simbu na wenzake watatu jana walifanyiwa bonge la pati pale makao makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlalakua, Dar es Salaam.

Hafla hiyo iliudhuriwa na viongozi mbalimbali wa JKT walioongozwa na Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyewapongeza wanamichezo hao ambao ni watumishi wa jeshi hilo.

Mbali na Simbu aliyerejea na medali ya shaba kutoka kwenye mashindano ya Dunia ya Riadha, wanariadha wengine waliokuwa kwenye mashindano hayo na kuandaliwa pati hiyo ni Stephano Huche, Emmanuel Giniki na Magdalena Shauri.

Simbu, aliishukuru JKT kwa kutambua mchango wao na kuahidi kupambana zaidi kuiletea nchi sifa katika mashindano mengine ya kimataifa.