Ikangaa kumbe naye yumo!

Muktasari:

Licha ya kuwa Mwanza kwenye Copa Umisseta, kumbe buana Kanali Mstaafu huyo alikuwa akifuatilia na mechi ya nusu fainali ya Simba kwenye Kombe la SportPesa kule Kenya.

UNAMKUMBUKA bingwa wa zamani wa Afrika wa mbio za marathoni? huyu ni Juma Ikangaa ambaye juzi aliibukia kwenye mashindano ya Copa Umisseta na alikuwa makini kufuatilia moja ya mechi za mpira wa kikapu jioni baada ya kushuhudia riadha asubuhi.

Licha ya kuwa Mwanza kwenye Copa Umisseta, kumbe buana Kanali Mstaafu huyo alikuwa akifuatilia na mechi ya nusu fainali ya Simba kwenye Kombe la SportPesa kule Kenya.

Sasa kilichotokea, wakati Simba inatinga fainali, Ikangaa akasema: “Jamani wakati mnaendelea huku, msisahau Simba katinga fainali kule Kenya”.

Hakuishia hapo akaendelea eti yeye si shabiki wa Simba, lakini kwenye mashindano hayo anaunga mkono timu za Tanzania za Simba na Singida United. Simba imetinga fainali na kesho Jumapili itacheza na Gor Mahia na Singida itavaana na Kakamega Homeboys kusaka nafasi ya tatu.

“Mimi si shabiki wa Simba wala Singida, lakini baada ya riadha napenda soka. Pia mimi ndiye niliyezianzisha timu hizi; JKT Tanzania na Transit Camp, kama ulikuwa haujui,” alisema.

Japo mwanariadha huyo alikataa kueleza katakata kilichomleta Mwanza kwenye Copa Umisseta, lakini taarifa zinasema amefika kuangalia vipaji sanjari na wadau wake wa riadha, Shirika la Maendeleo ya Japan (Jica).