Huyo kocha Zahera, kumbe amejipanga

Muktasari:

Zahera ambaye mchana wa leo Jumatatu atakuwa mbele ya waandishi wa habari nchini DR Congo akitangaza kikosi kitakachocheza mechi yao ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Nigeria, amewaambia mabosi wake akirejea anakuja na vifaa maalumu atakavyonunua kwa fedha zake vitakavyotumika kuwaumbua wachezaji wazembe atakaowaondoa.

KAMA mnamchukulia poa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera pole yako. Mkongo huyo bwana amejipanga kinoma kwani amepanga mara atakaporejea nchini kuanza rasmi kazi yake ya kuinoa timu hiyo, atatumia na vifaa matata vya kizungu.

Zahera ambaye mchana wa leo Jumatatu atakuwa mbele ya waandishi wa habari nchini DR Congo akitangaza kikosi kitakachocheza mechi yao ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Nigeria, amewaambia mabosi wake akirejea anakuja na vifaa maalumu atakavyonunua kwa fedha zake vitakavyotumika kuwaumbua wachezaji wazembe atakaowaondoa.

Kifaa hicho maarufu kama (GPS- Player Tek) kina uwezo wa kupima spidi na uwezo wa mchezaji katika kuhimili mikikimikiki kwa muda mrefu na Kocha Zahera ambaye mpaka sasa ameshakata mchezaji mmoja tu katika kikosi hicho, straika Donald Ngoma, katika listi nzima ya wachezaji waliosalia amesema kazi hiyo ataimalizia kirahisi mara baada ya kurejea akitokea Congo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika alisema Zahera amewaambia wala hataki klabu iingie gharama, hivyo anakwenda kununua vifaa maalumu vinavyotumika kupima uwezo wa kasi ya kukimbia ya mchezaji.

Nyika alisema Zahera anataka kubadilisha mambo mengi katika kikosi chao na anataka kujua kila mchezaji ana uwezo gani wa kukimbia na anataka kuona uwezo wa mwili wake kuwa tayari kwa mazoezi hayo na kuamua kuleta vifaa hivyo.

Alisema mara baada ya kuleta vifaa hivyo atavitumia kuangalia ubora wa wachezaji hao na watakaoonekana na uwezo mdogo wataondolewa haraka huku watakaosalia wataanza mazoezi makali ya kocha huyo.

Zoezi la kuwapima mara kwa mara litaendelea na kama watabainika wengine kushuka uwezo wanaweza kukatwa pia. “Kocha anaonyesha yuko siriazi kweli na kazi yake tulikutana naye kama kamati na akatuambia anaenda kwao, kule kuna vifaa maalumu atakavyorudi navyo, ili kutumia kuwapima wachezaji,” alisema Nyika. “Vifaa hivyo ni maalumu kupima uwezo wa mchezaji kukimbia, pia uwezo wa mwili wake kuweza kuhimili mazoezi ambayo atakuwa anayatoa, kilichotushangaza tulitaka tumsaidie kununua lakini ametuzuia amesema atakuja navyo mwenyewe.”

AZAM WA KWANZA

Vifaa hivyo ambavyo vinatumiwa na klabu kubwa Ulaya, hapa nchini kwa mara ya kwanza viliwahi kuhitajiwa na Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts lakini hakuvipata, ila Azam FC walivitumia chini ya Kocha Muingereza Stewart John Hall.

KINAVYOTUMIKA

Kifaa hicho ambacho kipo katika staili ya nguo aina ya vesti mchezaji hukivaa mwilini inawezekana ikawa ndani ya jezi yake ya juu au hata juu ya jezi ya mazoezi au mechi na ndani yake kuna kifaa maalumu kinachochukua takwimu za kasi ya mchezaji husika amekimbia kwa umbali gani na uwezo wa kasi yake kwa saa au dakika.

Mara baada ya mchezaji kumaliza mazoezi, mashine iliyopo ndani ya vesti hiyo huchukuliwa na kuonyesha takwimu zote katika kompyuta ambayo ndiyo inayokiendesha kifaa hicho na kutoa uwezo kamili wa kasi ya mchezaji.