Hivi Karia aliteleza au alidhamiria kwa Ninje?

Muktasari:

Vitu hivyo ni vya kipekee sana.

TANZANIA kuna mambo mengi ya kuvutia, kuanzia vivutio vya kitalii, vituko vya raia wake hadi baadhi ya kauli za viongozi wa kisiasa na wale michezo.

Vitu hivyo ni vya kipekee sana.

Ni kweli kabisa kuna baadhi ya mambo hutokea Tanzania tu, huwezi kuyakuta sehemu nyingine.

Mambo mengi yanayotokea Tanzania ni vigumu kuyasikia au kuyaona yakitokea katika nchi nyingine, hasa kwenye soka.

Huwezi kusikia kokote wachezaji tegemeo wa timu ya taifa wakiondolewa katika timu kwa ishu za ajira yake, ikizingatiwa ana uwezo wa kuibeba nchi kwenye michuano ambayo wanakwenda kushiriki.

Hilo limetokea Tanzania kwenye timu ya taifa ya riadha inayojianda kushiriki Michezo ya Madola. Inavutia sana!

Ni Tanzania tu ndipo kocha bora wa msimu, hatokani na bingwa wala timu za juu katika ligi ya ndani. Mbwana Makatta alipewa miaka miwili iliyopita kwa sababu tu aliiokoa Prisons isishuke daraja tena katika mechi tisa tu alizoiongoza timu hiyo.

Tanzania pekee inayoweza kumwita mchezaji wa timu ya taifa, bila kucheza kwa kipindi cha miezi sita mfululizo, lakini akaachwa mfungaji Bora anayetesa ughaibuni.

Kadhalika ni Tanzania inaweza kuahirisha mechi za Ligi Kuu Bara ili kuiruhusu timu moja shiriki kwenda kucheza ndondo nchi jirani. Yaani kila kitu ni manjegeka tu. Ukilishangaa hili, linaibuka jingine na wala hakuna anayejali. Raha iliyoje!

Hata wale waliosema, ukishangaa ya Mussa, utayaona ya Firauni, hawakukosea. Miezi mitatu iliyopita, timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilienda kushiriki Kombe la Chalenji Kenya.

Ilikuwa chini ya kocha aliyeibuka masikioni mwa mashabiki wa soka, Ammy Ninje ambaye kila sentensi zake mbili, lazima apige yai (atamke Kiingereza).

Uteuzi wa kocha huyo uliibua mijadala kama ilivyokuwa baada ya Kili kuchemsha vibaya katika michuano hiyo ikiwa imeambulia pointi moja tu katika mechi nne.

Juzi kati kocha huyo tena ameitwa na kupewa timu ya vijana ya umri wa chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ inayojiandaa na michuano ya kuwania fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika na Kombe Dunia 2019 kwa Vijana U20.

KILICHOSHTUA

Si tatizo kwa Kocha Ninje kupewa timu hiyo ya vijana kwa sababu huo ndio uwanja wake, hata kule England anakofundisha soka ni mahiri katika eneo hilo la soka la vijana kuanzia klabu ya Hull City mpaka Notts County FC.

Hata hivyo, kilichoshtua ni kauli ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliyemtaja Kocha Ninje kama mmoja kati ya mashujaa wawili wa soka la Tanzania na wanaoipaisha nchi barani Ulaya. Mwingine ni Mbwana Samatta.

TATIZO SIO SAMATTA

Kutajwa kwa Samatta kama shujaa wa Karia, haishangazi sana. Kwani ni vigumu kumkataa Samatta kuwa ni shujaa wa Tanzania kwa sasa kwa kuweza kuipaisha nchi na kuwa na manufaa kwa soka la Tanzania.

Kuanzia alipokuwa TP Mazembe akiwa Mtanzania wa kwanza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa 2015 hadi kunyakua tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wanaocheza ndani ya Afrika. Baadaye akatua KRC Genk ya Ubelgiji na ameendelea kuwa tegemeo la Tanzania.

Mabao yake yamekuwa yakiibeba Taifa Stars, mafanikio yake kisoka ni kichocheo cha nyota wengine wa soka Tanzania kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Saimon Msuva amekiri wazi kutua kwake Difaa El Jadida ya Morocco kuna mkono wa Samatta ambaye ni maarufu kwa majina ya Samagol na Popa. Kwanini Samagol asiitwe shujaa kwa kizazi hiki? Anastahili kabisa!

KARIA KATUZINGUA

Kama kuna jambo ambalo Karia amewashtua Watanzania ni kumtangaza Ninje kuwa Shujaa wa Tanzania kwa sababu tu, eti anazungumza vizuri Lugha ya Kiingereza na kuwanoa karibu nyota 15 wanaocheza Ligi Kuu ya England (EPL).

Kuna swali la kujiuliza hapa, nyota hao wanaocheza England ni Watanzania? Hapa Karia ni kama kawazingua watu na kutaka kuwaaminisha wadau wa soka kuwa, Ninje ni shujaa pasipo kufanya lolote la maana la kuudhibitisha ushujaa wake katika soka la Tanzania.

MSOMALI, KIBADENI JE?

Kama Ninje ni shujaa kwa kuwanoa nyota wa EPL, je, ingekuwaje kwa mtu kama marehemu Athuman Kilambo, Mohammed Msomali, Abdallah Kibadeni ama Joel Bendera (marehemu) waliowaibua nyota waliotikisa ndani na nje ya Tanzania, hawa wangeitwaje?

Kama Ninje ni shujaa kwa sababu ya kufundisha soka Ulaya, vipi kwa Sunday Manara aliyeanza kucheza soka la kulipwa barani Ulaya tena katika nchi zilizotikisa duniani kama Uholanzi na kwingine miaka ya 1970 angetukuzwaje?

Iwapo Ninje ni shujaa kwa sababu ya kufundisha England, Paul West Gwivaha na Joel Bendera walioipeleka Tanzania kwa mara ya kwanza na mwisho katika fainali za Kombe la Afrika (Afcon 1980) wangeitwa kina nani? Kama ni shujaa, Peter Tino aliyeipeleka Tanzania Fainali za Afrika 1980 kule Lagos, kwa bao lake, tumwiteje?

Kwa hakika kauli hii ya Karia inashangaza kama yanavyoshangaza mambo mengine yanayotokea Tanzania tu na aslani huwezi kuyaona wala kuyasikia kwingineko.

ILA FRESHI

Tunajua wakati mwingine ukiwa kiongozi wa taasisi kuna maswali yanakera, lakini Karia alipaswa kujua Watanzania wana upeo mkubwa wa soka la Tanzania kuliko anavyotaka kuwalazimisha watu waelewe ishu ya Ammy Ninje.

Inafahamika Ninje ni swahiba wa mmoja wa viongozi wa TFF na hata uteuzi wake tangu wa Kili Stars mpaka huu wa sasa wa Ngorongoro Heroes unatokana na uswahiba huo mbali na wasifu alionao na unaoongezewa chumvi.

Hivyo, Karia wala hakuwa na haja ya kuzunguka sana na kumpamba kocha huyo, kwa sababu kila kitu kipo wazi na Watanzania ni waelewa.

Hata hivyo, muhimu kwa Karia kama alivyouliza mwenyewe; ‘Watanzania mnataka nini nyie?’ Ajue wazi Watanzania wanataka matokeo bora ya mechi za timu ya taifa, iwe Taifa Stars ya Salum Mayanga ama Ngorongoro Heroes ya Ninje na nyinginezo.

Kama Ngorongoro itashindwa kupata matokeo mazuri fainali za Kombe la Dunia 2019 zitakazofanyika Poland kupitia Afcon U20 ya hapo Niger, basi Karia ajiandae tu kuumbuka na shujaa wake, Ammy Ninje. Hakika muda utathibitisha tu kauli yake, ila kama aliteleza katika kauli yake, ni bora aombe radhi kwani huenda alipitiwa na kuisahau historia ya soka la Tanzania na aina ya wanamichezo wanaostahili kuwa mashujaa wa soka la Tanzania.imefikisha.