Haya sasa, mbio za mbuzi hizoo zimefika

KAMA hutaki shauri yako, lakini mbuzi nao wana mbio zao ambazo msimu huu zitafanyika keshokutwa Jumamosi kwenye eneo la The Green lililopo Barabara ya Kenyatta, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti Mwenza wa mbio hizo, Rachel Carlin, amesema wanalenga kukusanya Sh120 milioni ambazo zitasaidia shughuli mbalimbali za jamii.

“Mbio zitaanza saa 6:00 mchana na kumalizika saa 11:15 jioni, hizi ni mbio maalumu kwa ajili ya kusaidia jamii na tangu zimeanza tumeshakusanya zaidi ya Sh1 bilioni ambazo zilipelekwa kusaidia jamii,” alisema Carlin.

“Msimu huu kiingilio kitakuwa Sh20,000 kwa watu wazima na Sh10,000 kwa watoto, lakini wale wenye umri chini ya miaka mitatu ni bure.”

Kwa mujibu wa Carlin, wao kwa kushirikiana na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Coca Cola kwanza, Toyota Tanzania, Hoteli ya Southern Sun, Shirika la Ndege la Uswisi na Benki ya Stanbic, wameboresha zaidi mbio hizo.