Hawa ZFA wakizingua tu, inakula kwao mapemaaa

Ravia Idarous Faina

Muktasari:

  • Rais Ravia Idarous Faina na makamu wake Ali Mohamed kutoka Pemba na Mzee Zam Ali wa Unguja waliandika barua za kujiuzulu kutokana na kashfa ya kupelekwa wachezaji vijeba katika mashindano ya Cecafa U17 yaliyofanyika Burundi.

SIKU moja tu baada ya Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kuwagomea mabosi wao wa juu kujiuzulu nafasi zao, Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Soka Zanzibar imepinga uamuzi huo ikitaka wazingatie kujiuzulu kwa viongozi hao.

Rais Ravia Idarous Faina na makamu wake Ali Mohamed kutoka Pemba na Mzee Zam Ali wa Unguja waliandika barua za kujiuzulu kutokana na kashfa ya kupelekwa wachezaji vijeba katika mashindano ya Cecafa U17 yaliyofanyika Burundi.

Mrajis Suleiman Pandu Kweleza alisema ofisi yake inatambua uhalali wa kujizulu viongozi hao ambao waliandika barua wenyewe kujiweka pembeni kwa sababu wanazozifahamu na kushangaa kusikia Kamati ya Utendaji ya ZFA ikigomea suala hilo.

Alisema hakubaliani na uamuzi wa kamati hiyo kutaka kuwarejesha madarakani wakati waliachia ngazi wenyewe bila kulazimishwa.

Aidha alisema kutokana na viongozi hao kujiuzulu wenyewe ofisi yake imeiandikia barua chama hicho juu kuweza kuandaa katiba mpya itakayofuta makosa yote ya nyuma na kuifanya ZFA ifanye kazi zake kwa ufanisi.

“Ofisi yangu imeshachukua hatua ya kupelekea barua ZFA juu ya kuhakikisha kwamba wanawasilisha katika mpya ambayo itaboreshwa zaidi ili iwe na utofauti na iliyopo,” alisema.

Pia aliitaka Kamati ya Utendaji za ZFA kuitisha haraka uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya waliojiuzulu ikiwa ni utekelezaji wa katiba ya chama hicho.