Cheki Messi alivyokuzwa na sindano za sh100,000 kwa siku

PAUL Pogba alijipimisha kimo na Lionel Messi walipokutana kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2015, akamwona Muargentina huyo dogo tu kwake.

Lakini, mechi ilipoanza akaona ufundi wa dogo huyo na kuishia kusema ‘Acheni Messi aitwe Messi’.

Pogba alisema mpira uliochezwa na Messi fainali hiyo na ule anaoendelea kuucheza siku zote, hakuna mwingine anayeweza kufanya hivyo.

Siku hiyo, Juventus ya Pogba ilichapwa mabao 3-1. Messi hakufunga, ila shughuli yake na namna alivyokuwa akiwachambua wachezaji katikati ya uwanja, ilidhihirisha ni wa daraja la juu zaidi.

Kimo cha Messi hakiendani na mambo anayoyafanya ndani ya uwanja. Staa huyo wa Barcelona ameripotiwa alipokuwa mdogo alikumbwa na tatizo la kihomoni, lililomfanya ashindwe kurefuka zaidi na ndiyo maana ana kimo hicho, futi 5 na inchi 7.

Messi mwenyewe anafichua kile alichokifanya huko utotoni hadi kumfanya afanikiwe kupata kimo hicho alichonacho kwa sasa, la sivyo hali ingekuwa mbaya zaidi.

Pengine Messi angekuwa mfupi zaidi na hilo lingemtibulia kisoka.

Katika mahojiano na America TV, Messi amefichua kila kitu, kwamba ilibidi ajichome sindano ya homoni kila siku kuanzia akiwa na miaka minane hadi alipofikisha miaka 14 ili kupata kimo alichonacho sasa.

Messi anasema mwanzoni wazazi wake ndio waliokuwa wakimchoma sindano hizo miguuni kila siku usiku na alipofikisha miaka 12 alianza kujichoma mwenyewe.

Messi alikumbwa na tatizo la kukosa homoni za kumfanya arefuke wakati alipokuwa kwenye mji wa kwao, Rosario, Santa Fe, Argentina.

“Nilikuwa najichoma sindano kwenye miguu mara moja kila usiku. Nilianza kujichoma mwenyewe nikiwa na umri wa miaka 12, si jambo nilililokuwa nikilifurahia,” alisema Messi.

“Huko nyuma wazazi wangu ndio waliokuwa wakinichoma hizo sindano tangu nikiwa na umri wa miaka minane na walinifundisha ili nianze kujichoma mwenyewe. Sindano haikuwa ikiuma, kwa sababu ilikuwa ndogo na nilikuwa najichoma kawaida tu.”

Wazazi wake walikuwa wakizigharimia sindano hizo za Messi, Pauni 1,069 kwa mwezi, sawa na Sh3,369,340 za Kitanzania, ikiwa ni zaidi ya Sh100,000 kwa siku.

Baadaye, klabu yake ya zamani, Newell’s Old Boys, ilichukua majukumu ya kulipia gharama hiyo ya sindano za Messi.

Mwaka 2001, akiwa na umri wa miaka 13, Messi na familia yake walihamia Barcelona na klabu hiyo ilikubali kulipia gharama zote za matibabu yake hadi dozi yake ya sindano ilipofika mwisho alipokuwa na umri wa miaka 14.

Gwiji huyo wa Barcelona alisema: “Halikuwa jambo gumu kabisa kwangu kuja Barcelona. Mimi niliyazoea mazingira kwa haraka sana, lakini familia yangu ilishindwa kufanya hivyo. Ndugu zangu walitaka kurudi nyumbani Argentina na walifanya hivyo.

“Barcelona tulibaki mimi na baba tu na kuna siku moja aliniuliza ‘tunafanyaje?’ Nilimjibu baba yangu ‘mimi nataka kubaki’.”

Ndipo hapo staa huyo alipobaki Barcelona, mahali ambako anacheza soka la kiwango bora na kuvunja rekodi kibao zilizowahi kuwekwa kwenye mchezo huo duniani.

Akitoa huduma yake kwenye kikosi hicho, Messi amefanikiwa kubeba tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia mara tano na kuwa mmoja wa wachezaji wanaotajwa kuwa ni bora kuliko yeyote aliyewahi kutokea katika mchezo wa soka duniani.

Shida ya kukua haikuwa tatizo kwa Messi na kumfanya aendelee kucheza soka maridadi, akifunga mabao 374 katika mechi 410 alizoichezea Barcelona kibingwa.

Messi amekiri wasiwasi wake kuhusu kurudi Argentina wakati atakapostaafu soka huko Barcelona ikiwa ni sehemu tu ya kubainisha kile anachotamani kukifanya baada ya soka lake huko Nou Camp.

Messi ameifanya Barcelona kuwa moto msimu huu ikielekea kubeba taji la La Liga baada ya kuweka pengo la pointi 11 katika msimamo wa ligi hiyo.

Barcelona ipo kwenye robo fainali pia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo itakipiga na AS Roma ya Italia, huku wakiwinda pia rekodi yao ya kunyakua mataji matatu makubwa kwa msimu huu kwa sababu wanalisaka pia taji la Copa del Rey.