Bondia Nyilawila autaka ubosi wa ndondi

Friday January 12 2018

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Bondia Karama Nyilawila amepanga kutundika glovusi baada ya pambano lake la Julai 27 la nchini India, lakini ataondoka kwenye masumbwi moja kwa moja kwani anafikiria kujitosa kuwania uongozi wa bodi ya ngumi.

Serikali iko mbioni kuunda bodi itakayosimamia masuala yote ya ngumi za kulipwa nchini na tayari kamati ya kuratibu mchakato huo imeteuliwa na Januari 31 itawasilisha mapendekezo yao kwa Waziri wa Habari,Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

"Nahitaji kuwa kiongozi wa ngumi, uwezo huo ninao na nimaamini mchango wangu utasaidia kuziweka mahali pazuri ngumi zetu," alisema Nyilawila na kufafanua kuwa ataanza mchakato huo baada ya pambano lake la India.

"Nakwenda India kucheza pambano na bondia wa nchini humo, hilo ndilo litakuwa pambano langu la mwisho kupigana kisha nastaafu kupigana," aliongeza.

Nyilawila aliwahi kuwa bingwa wa dunia wa WBF baada ya kushinda nchini Russia anaendelea na mazoezi kwenye gym ya Chid Kinondoni kujiweka fiti kwa pambano hilo.