Bizimungu kacharuka, ashusha hasira kwa JKT

Muktasari:

  • Bizimungu alisema matarajio yao yalikuwa ni kubaki na pointi tatu katika uwanja wao wa nyumbani, lakini makosa ya safu yake ya ushambuliaji na kukosa umakini kwa mabeki yaliwagharimu.

BAADA ya Mwadui FC kutoshana nguvu ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Azam, imeonekana kumkera Kocha wa timu hiyo, Ally Bizimungu na kusisitiza mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania watamalizia hasira zote kwa maafande hao.

mchezo wa juzi ulikuwa wa kwanza kwa Mwadui kukipiga katika dimba la nyumbani na kujikuta wakibanwa mbavu kwa kugawana pointi na Azam.

Bizimungu alisema matarajio yao yalikuwa ni kubaki na pointi tatu katika uwanja wao wa nyumbani, lakini makosa ya safu yake ya ushambuliaji na kukosa umakini kwa mabeki yaliwagharimu.

Aliongeza kuwa mapungufu aliyoyaona kikosini, atahakikisha anakaa na vijana wake ili yasijitokeze katika mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania na kuvuna ushindi.

“Tuliamini lazima tushinde, lakini makosa ya washambuliji wangu na mabeki kukosa umakini ndio yalitugharimu kwahiyo tunaenda kujipanga na JKT Tanzania kuhakikisha tunashinda,” alisema Bizimungu.

Straika Ibrahim Irakoze ambaye alipiga shuti akiwa nje ya 18 na kuzaa bao lililofungwa na Edwin Innocent dakika ya 71 alisema watazidi kujipanga katika michezo ijayo.

Azam ndio walikuwa wa kwanza kufumania nyavu katika mchezo huo kwa bao la Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ dakika ya 55.

Alisema kikubwa anachotaka ni wachezaji kutokukata tamaa na matokeo waliyoyapata wayachukulie kama changamoto ya kufanya vyema kwenye michezo inayofuata.