Bakhresa azuiwa

Muktasari:

Ingawa wahusika wamesisitiza kuwa ni uzushi, habari mbaya kwa watu wa Simba ni kwamba hata kama ingekuwa ni kweli Bakhresa ana nia hiyo, vigezo vya leseni kwa klabu zilizowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) vinamzuia kwani tayari anamiliki klabu ya Azam FC.

MCHAKATO wa mabadiliko ndani ya klabu ya Simba umefikia patamu na leo Jumanne, klabu hiyo itaweka hadharani idadi ya ofa walizopokea mpaka sasa, lakini gumzo kubwa ni taarifa za kwenye mitandao kuwa Bilionea, Said Salim Bakhresa naye yumo.

Ingawa wahusika wamesisitiza kuwa ni uzushi, habari mbaya kwa watu wa Simba ni kwamba hata kama ingekuwa ni kweli Bakhresa ana nia hiyo, vigezo vya leseni kwa klabu zilizowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) vinamzuia kwani tayari anamiliki klabu ya Azam FC.

KANUNI INASEMAJE?

Kifungu cha 11 (J3) cha leseni za CAF za klabu kinasema. “Mwombaji wa leseni anatakiwa kuwasilisha hati ya kiapo ikionyesha kuwa hana uhusiano au mgongano wowote wa maslahi na timu nyingine, kiutawala, kiusimamizi na katika ufanisi wa timu nyingine, moja kwa moja ama kwa njia yeyote ile.” Kifungu kidogo cha (e) kinasema; “Anatakiwa kuthibitisha kuwa siyo mwanachama ama mhusika wa timu nyingine inayoshiriki katika mashindano hayo hayo.”

KAZI NZITO

“Utaratibu wa leseni kwa klabu hauruhusu mtu mmoja kumiliki timu zaidi ya moja. Hata kama atasema nyingine ni timu ya watoto wake, bado atakuwa na ushawishi, leseni inakataza hivyo. Hili linambana Bakhresa kuwekeza Simba kwani, anamiliki Azam FC,” alisema kigogo mmoja wa Bodi ya Ligi.

Naye Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema hawezi kuzungumzia suala la Bakhresa kwani, bado halijawa rasmi, lakini aliweka wazi namna mchakato wa leseni unavyofanya kazi.

“Mchakato wa leseni za klabu unataka kuondoa mgongano wa maslahi. Mfano unakuta timu inamilikiwa na taasisi tofauti, lakini juu yake zinaendana kwa namna fulani. Yaani mtu wa timu moja anakuwa na nguvu kwingine, hilo halitakiwi,” alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Zabuni Simba, Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo alisema habari za Bakhresa na wengine wanaotajwa ni za mtaani kwa kuwa utaratibu wa tenda hauruhusu kufahamika kwa walioweka nia na hufanywa kwa siri kubwa.

“Utaratibu uliopo hauruhusu hizo ofa kufunguliwa mpaka kamati maalum iliyoundwa kuzichambua ikae, hivyo hizo taarifa za watu wanaotajwa kuwekeza ni za mtaani tu, tusubiri wenye mamlaka wafanye kazi zao,” alisema Jaji Mihayo.

“Mchakato wa zabuni una taratibu zake, baada ya tarehe 18 kamati hiyo maalum itazichambua hizo tenda na kuona waliokidhi vigezo, kisha mchakato unaendelea katika awamu ya pili mpaka mwisho ndiyo tutafahamu aliyeshinda,” alifafanua zaidi.

Katibu Mkuu wa Simba, Dk. Anord Kashembe alisema leo Jumanne klabu yao itatangaza walipofikia katika mchakato huo, ili kupata taswira halisi ya namna mambo yanavyokwenda.

Katika mchakato huo wa mabadiliko, mwekezaji atapewa asilimia 50 ya umiliki kwa kiasi kisichopungua Sh20 bilioni huku asilimia nyingine zikibaki kwa wanachama ambapo kwa kuanzia, watagawana asilimia 10 na kuhifadhi nyingine 40. Awali, bilionea Mohammed Dewji ‘MO’ alitangaza nia ya kununua asilimia 51 ya hisa kwa Sh20 bilioni.