Bakayoko aonyeshwa mlango wa kutokea Chelsea

Muktasari:

  • Mchezaji huyo alisajiliwa kiangazi cha mwaka jana akitarajiwa kuwa mrithi wa Nemanja Matic aliyetimkia Manchester United.

London, England. Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri, amemwambia wazi kiungo wake Tiemoue Bakayoko kuwa ameshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mchezaji huyo alisajiliwa kiangazi cha mwaka jana akitarajiwa kuwa mrithi wa Nemanja Matic aliyetimkia Manchester United.

Bakayoko alishindwa kujihakikishia nafasi chini ya kocha aliyemsajili Antonio Conte, tangu kutua kwa Sarri, nafasi ya Bakayoko imekuwa shakani na ameambiwa aende atakako.

Chelsea inatarajiwa kushuka dimbani kuanza kusaka taji la Ligi Kuu England itakaposafiri kuifuata Huddersfield.

"Nadhani baadhi ya wachezaji wetu walioshindwa kujihakikishia namba wanaweza kwenda popote kwa mkopo, ninahitaji wachezaji 23 au 24 nitawaongezea chipukizi watatu au wane kutoka timun ya vijana,” alisema.

Aidha Sarri ametangaza kuwa Cesar Azpilicueta ndiye atakuwa nahodha wa kikosi cha Chelsea katika mchezo wa leo na bado hajafahamu kama unahodha huo utaishia kwenye mechi hiyo ama laa.

Sarri pia alisema bado anayumba hajajuwa nani atasimama langoni katika mchezo wa leo ni kipa wake ghali Kepa Arrizabalaga ama atasimama mkongwe Willy Caballero katika mechi itakayopigwa uwanja wa Kirklees.