Ajibu agawa laki mbili mbili Yanga

Muktasari:

Sasa Yanga inashika nafasi ya nne na pointi hizo nane, nyuma ya Mtibwa Sugar, Simba, Azam FC na Tanzania Prisons.

MSHAMBULIAJI Ibrahim Ajib ndiyo amefunga mabao mawili kati ya manne ya kikosi cha Yanga na mabao hayo ndiyo yaliipa pointi sita kati ya nane walizonazo.

Ushindi wa mechi hizo umewapa Sh200,000 kila mchezaji wa timu hiyo huku zile walizopata sare wakiambulia Sh100,000 kwa zote mbili.  Katika michezo minne ambayo Yanga wamecheza, walitoa sare ya 1-1 na Lipuli ya Iringa bao alifunga Mzambia Donald Ngoma ambaye alifunga tena kwenye sare ya 1-1 na Majimaji, wakati Ajib alifunga bao katika ushindi wa 1-0 na Njombe Mji, Njombe na walipoipiga Ndanda 1-0, Dar es Salaam. Ajib amesisitiza mapambano bado yanaendelea na ana imani watakaa sawa huku akiushukuru uongozo kwa jitihada zao.

Hata hivyo, Yanga yenye washambuliaji kama, Mzambia Obrey Chirwa, Matheo Antony na Geofrey Mwashiuya, ilikuwa inakosa huduma ya mshambuliaji wake Mrundi Amissi Tambwe ambaye alikuwa majeruhi.

Sasa Yanga inashika nafasi ya nne na pointi hizo nane, nyuma ya Mtibwa Sugar, Simba, Azam FC na Tanzania Prisons.

Posho zinavyokuwa

Ofisa habari msaidizi wa Yanga, Godlisten Anderson alithibitisha jana wamejipanga na ndio maana wamehakikisha masilahi ya wachezaji yanakaa sawa.

“Kila mechi itatoka pesa, kama wachezaji wakipata ushindi kila mmoja anapata laki moja,” alisema Anderson na kuongeza timu ikipata sare ugenini hupata nusu ya posho ya ushindi lakini wakitoa sare Dar es Salaam hawapewi kitu.

Tambwe karudi

Straika hatari wa Yanga Amiss Tambwe alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya goti ambayo aliumia akiwa katika maandalizi ya msimu huu wa Ligi Kuu Bara huko Visiwani Zanzibar.

Habari njema kwa mashabiki wa Yanga Tambwe anaanza matizi leo Jumatatu ya kujianda na mechi ijayo ya ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo itachezwa wiki ijayo.