Afrika macho kodo kwa mastaa hawa

UNAAMBIWA hivi, Fainali za Kombe la Dunia zinapofika ni mahali pengine mwafaka pa kutafutia dili tamu za pesa nyingi kuhusiana na usajili kwa mchezaji.

Wapo mastaa walionasa dili za maana na kusajiliwa na timu kubwa baada ya kufanya vyema kwenye fainali za Kombe la Dunia kama ilivyotokea kwa Mesut Ozil, aliyenaswa na Real Madrid baada ya Kombe la Dunia 2010 Afrika Kusini, alipoupiga mpira mwingi akiwa na Ujerumani au El Hadji Diouf aliponyakuliwa na Liverpool baada ya kutamba na Senegal kwenye Kombe la Dunia 2002 huko Korea Kusini na Japan.

Mastaa wa kutoka nchi za Ulaya wanaotazamiwa kwenda kuonyesha ubabe kule Russia ni pamoja na washambuliaji matata kabisa kama Harry Kane wa England, Robert Lewandowski wa Poland, Cristiano Ronaldo wa Ureno, Antoine Griezmann wa Ufaransa na mkali kama Thomas Muller wa Ujerumani.

Kwa upande wa viungo ndio usiseme kabisa, kuna wakali kama Paul Pogba, Toni Kroos, Sergio Busquets, Isco, Bernardo Silva, Dele Alli, Mousa Dembele na wengine kibao ambao watakuwa na shughuli ya kuonyesha ubabe tu na wakali wengine.

Amerika Kusini, utataja mataifa makubwa matupu ambayo yameendelea kisoka kama vile Argentina, ambayo itakuwa na mastaa kibao wakiongozwa na Lionel Messi, wakati Brazil mastaa wao wataongozwa na Neymar huku huko Uruguay kuna wakali kama Luis Suarez na Edinson Cavani. Huo ndio utamu wa fainali za Kombe la Dunia.

Lakini, yote kwa yote, macho ya Waafrika wengi yatakuwa kwa wawakilishi wa bara hilo kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia huko Russia kuona ni staa gani atakuwa kinara wa kulipaisha taifa lake na kuhakikisha linafanya vyema?

Mataifa matano yatakaoiwakilisha Afrika kwenye michuano hiyo, kila moja ina staa wake na macho ya wengi yatakuwa kwa wakali hawa kuona ni kitu gani watafanya kuwatesa wazungu na mabara mengine yatakayochuana kwenye mikikimikiki hiyo ya kumsaka bingwa wa dunia.

Mohamed Salah, Misri

Kwa kiwango cha Mohamed Salah kwa msimu huu, pengine kama angekuwa mfanyabiashara basi chochote ambacho angeweka mezani kingepata mteja. Amekuwa moto kweli na Ligi Kuu England na Ulaya wanamfahamu vyema kwa ile huduma yake anayotoa huko Liverpool.

Huu ni msimu wake wa kwanza huko Anfield, lakini ameshavunja na kuweka rekodi kibao ikiwamo ya kufunga mabao 32 Ligi Kuu England, ikiwa ni rekodi kwa mchezaji kufunga mara nyingi hivyo ndani ya msimu mmoja wenye mechi 38. Salah kwa ujumla amepiga mabao 44, huku kiwango chake kikimfanya aanze kuwekwa kwenye anga moja na mastaa kama Messi na Ronaldo licha ya kwamba, mwenyewe hataki. Amepachikwa jina la Mfalme wa Misri huku kiatu chake kikiwekwa makumbusho, lakini kubwa linalosubiri kama moto wake utawaka huko Russia.

Sadio Mane, Senegal

Kama umekuwa ukinogewa na ile fowadi ya Liverpool msimu huu na kumpa burudani kocha Jurgen Klopp, basi mmoja wa wachezaji wanaounda safu hiyo, yupo Msenegali, Sadio Mane. Asikwambie mtu, shughuli ya Mane imemfanya Salah kuwa na kazi moja tu ya kusukumia mipira wavuni kwa sababu mambo mengine yote magumu yamekuwa yakifanywa na Mane na mwenzake Roberto Firmino.

Kuthibitisha umuhimu wa Mane huko Anfield ni mkubwa unakuja hapa, wakati ukishangilia mabao ya Salah kwa msimu huu, lakini saba yametokana na pasi za Mane.

Senegal itakwenda Russia na macho ya mashabiki wake yatakuwa kwa Mane, ambaye ndiye anayebeba tumaini ya Simba wa Teranga.

Wahbi Khazri, Tunisia

Moja ya silaha kule Russia ipo kwa kiungo mshambuliaji, Wahbi Khazri. Hakuna asiyefahamu mchango wa staa huyo kwenye kikosi chake cha timu ya taifa. Khazri ilikuwa ngumu kucheza kwenye daraja la chini huko Sundarland na hivyo, alipelekwa kwa mkopo Rennes ya Ufaransa inayoshiriki ligi.

Kuonyesha kwamba ubora wake umemfanya awe kwenye kikosi hicho alichopo kwa sasa, Khazri kwenye kikosi cha Tunisia amepita kwenye vikosi vyote kuanzia timu ya vijana na sasa atavikwa majukumu ya kuhakikisha nchi yake inatoboa na kuvuka hatua ya makundi katika michuano hiyo ili kuwafanya Waafrika kuwa na sababu ya kushangilia timu zao zitakazochuana katika mikikimikiki ya kusaka ubingwa wa dunia.

Victor Moses, Nigeria

Antonio Conte tangu alipotua kwenye kikosi cha Chelsea amemfanya Mnigeria, Victor Moses kuwa mchezaji muhimu kweli kweli na kuboresha ubora wake uliomfanya kuwa mchezaji mkubwa. Wakati fainali za Kombe la Dunia zikitarajia kuanza huko Russia, Nigeeria ni nchi yenye vipaji vingi vya wanasoka, lakini hakuna ubishi watahitaji staa mwenye uzoefu wa kucheza mechi ngumu kama ilivyo kwa Victor Moses. Wakati Super Eagles ikitarajiwa kuwa na damu changa nyingi kwenye michuano hiyo ya Kombe la Dunia kama vile Alex Iwobi, Kelechi Iheanacho na Wilfried Ndidi, staa kama Victor Moses ni chaguo muhimu kuhakikisha Nigeria inakuwa na utulivu kwenye kikosi chake na kufanya mambo mazuri ndani ya uwanja ili kuleta matokeo mazuri kwa Bara la Afrika.

Mehdi Benatia, Morocco

Beki kisiki huyu, amekuwa na uzoefu wa muda mrefu akichezea klabu za Ulaya. Pale Juventus kwa sasa ndiyo mlinzi muhimu zaidi amekuwa na mchango mkubwa sana akiiwezesha timu hiyo kufika katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini pia kunyakuwa kwa mara nyingine taji la Seria A kwa mfululizo. Pale Morocco uongozi wake utakuwa chachu ya kupambana kwa ajili ya taji hilo la dunia kuweza angalau kufika hatua za juu. Ni wazi kabisa macho ya mashabiki wa soka wa Afrika watakapoitazama Morocco wataona mastaa wengi, lakini Benatia atakuwa mchezaji muhimu kabisa ambaye wataamini ataokoa jahazi na kama akifanya hovyo basi watu waliowengi watashangaa.