Liverpool sasa iko kamili, yaichapa Torino

Liverpool, England. Klabu ya Liverpool, imemaliza mechi za kujipima nguvu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya kwa ushindi wa kishindo wa mabao 3-1 dhidi ya Torino ya Italia, mchezo uliochezwa jana usiku dimbani Anfield.

Kiungo Fabinho, alishindwa kuifungia Liverpool bao la kuongoza alipokosa mkwaju wa penalti  iliyotokana na Sadio Mane kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Kocha Jurgen Klopp, ambaye alikianzisha kikosi imara alifurahia pale kiungo wake Roberto Firmino akiifungia timu yake bao la kuongoza mapema kabla ya nyota huyo kutoka Brazil kufunga la pili ndani ya dakika 45.

Kiungo wa Kiholanzi Georginio Wijnaldum aliifungia Liverpool bao la tatu huku kipa mpya wa timu hiyo mbrazil, Alisson akionekana kufanya vizuri langoni, mpira pekee uliomshinda kuudaka ni ule wa kichwa uliopigwa na Andrea Belotti aliyeifungia Torino bao la kufutia machozi.

Ushindi huo unawaweka Liverpool katika hali nzuri wanapoisubiri West Ham United katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England mchezo utakaopigwa Anfield.

Kocha Klopp anasubiri kuona kiwango cha wachezaji wake waliokuwa majeruhi kwa kipindi kirefu msimu uliiopita na nyota wapya ambao sasa wapo fiti ambao ni Daniel Sturridge, Adam Lallana, Danny Ings na Marko Grujic, mchezaji mpya ni Xherdan Shaqiri.