‘Jembe Ulaya’ awafunda mastaa wa Yanga SC

Arusha: Beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, amewataka wachezaji wa timu hiyo kutekeleza majukumu ya kazi na kuweka kando mgogoro wa uongozi.

Akizungumza mjini hapa, Malima alisema Yanga inapitia kipindi kigumu kiuchumi, lakini wachezaji wanapaswa kujiepusha na mgogoro unaofukuta ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Beki huyo alisema wachezaji wanatakiwa kuwa wavumilivu na kuweka mbele masilahi ya Yanga kwa kucheza mpira katika mashindano yanayowakabili.

Alisema licha ya kuyumba kiuchumi, wachezaji wanatakiwa kuongeza kasi ya mazoezi na kushinda mechi mbili zijazo za kimataifa dhidi ya USM Alger na Rayon Sports ya Rwanda.

“Wachezaji wanatakiwa kubaki na msimamo wa kazi yao sio kuingilia mgogoro usiowahusu, wao kazi yao ni kucheza na kujitangaza ili wafike mbali hasa katika michezo ya kimataifa wanayoshiriki,”alisema Malima.

Aidha, Malima alisema Yanga inapitia kipindi kigumu na amewataka wanachama kujifunza kupitia mgogoro uliochangia timu hiyo kutopata matokeo mazuri katika mashindano ya kimataifa.

Alisema wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wanatakiwa kuwaunga mkono viongozi ili kujenga timu imara ambayo itashindana kikamilifu katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopangwa kuanza Agosti 22.

“Yanga wanajimaliza wenyewe hakuna mtu wa kumlaumu na wasipokuwa makini watazidi kujiongezea matatizo migogoro mingine haina maana. Hakuna sababu ya kunyoosheana vidole jambo la msingi ni kujenga umoja,” alionya Malima.

Nguli huyo alionya Yanga isipokuwa makini itakosa viongozi bora kwa kuhofia migogoro ndani ya klabu hiyo kongwe kutoka makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam