Lampard kama Gerrard unaambiwa

Muktasari:

Hata hivyo, hiyo sio ishu sana kama vipi ipotezee tu. Iko hivi kiungo wa zamani wa Chelsea aliyeipa mafanikio kibao, Frank Lampard anakaribia kunasa kibarua cha kuinoa Derby Country

Alitajwa sana kuingizwa kwenye benchi la ufundi la Chelsea, ambayo msimu huu imekuwa na majanga kwelikweli katika Ligi Kuu England. Lakini, angalau wachezaji watakuwa wamempa mkono wa kwaheri bosi wao, Muitaliano Antonio Conte ambaye ana dalili zote za kutupiwa virago, kwa kushinda taji la FA tena kwa kuichapa Manchester United ya Jose Mourinho.

Hata hivyo, hiyo sio ishu sana kama vipi ipotezee tu. Iko hivi kiungo wa zamani wa Chelsea aliyeipa mafanikio kibao, Frank Lampard anakaribia kunasa kibarua cha kuinoa Derby Country.

Tajiri wa timu hiyo Mel Morris, anataka kuona kazi ya kuwanoa wachezaji wake msimu ujao inafanywa na Lampard na tayari mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya kiungo huyo mwenye mashuti na pasi zilizonyooka anatua Pride Park.

Kabla ya dili hilo, Lampard pia alikuwa akihusishwa na kupewa jukumu la kuinoa timu nyingine ya Daraja la Kwanza ya Ipswich Town, lakini walishindwa kufikia makubaliano kwenye suala zima la mkwanja.

Hata hivyo, mbali na Lampard, wengine ambao wanahusishwa na kupewa kibarua hicho ni kocha wa Brentford, Dean Smith, Alex Neil wa Preston, Paul Cook anayeinoa Wigan na Neil Harris wa Millwall.

Lampard, 39, ana leseni ya ukocha wa daraja A jambo ambalo linawapa mzuka wamiliki wa timu mbalimbali kumpa kazi wakiwa na uhakika timu zao zitakuwa maarufu na kusonga mbele.