NMB Korogwe yasaidia Umisseta

Korogwe;  Benki ya NMB Korogwe imewafuta machozi wanamichezo wanaojiandaa na mashindano ya Umiseta kwa kuwapatia msaada wa maji safi ili yaweze kuwasaidia kwenye kambi yao waliyoiweka Mji wa Hale wilayani Korogwe.

Makabidhiano ya msaada huo yamefanyika kati ya Meneja wa NMB Korogwe, Lugano Mwampeta na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Dk George Nyaronga.

Mwampeta amesema, wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao kama wafanyakazi katika kusaidia huduma za jamii.

"Tunachokifanya hapa ni kuwapatia mchango wetu wenzetu wa halmashauri ya wilaya, ni kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu walioweka kambi kule mjini Hale," amesema Meneja huyo wa NMB.

Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Korogwe, Patricia Mbigiri amewashukuru wafanyakazi wa benki ya NMB kwa msaada huo na ametoa rai kwa watu wengine wajitokeze kuwasaidia.

Mbigiri amesema kuwa wanamichezo hao waliopiga kambi ya mazoezi mjini Hale wanajiandaa na mashindano yatakayofanyika  Tanga na ametoa wito kwa wapenzi wa michezo kuunga mkono maandalizi.

Amesema, michezo ni ajira, husaidia kujenga afya ya jamii na pia kuwajenga kisaikolojia wanafunzi hao hivyo kuwa rahisi kwao kufaulu mitihani yao na kuelewa vyema masomo yao ya kila siku wanayofundishwa wakiwa darasani.