Awesu, Chalamanda wamepambana bwana

SIMBA imeshatwaa taji la Ligi Kuu Bara. Njombe Mji imeshuka daraja. Nini kimebaki sasa?

Ni mambo machache tu. Msimu ndio unakaribia kufika ukingoni na kila timu pamoja na wachezaji wamevuna walichokipanda ikiwa ni pamoja na kufanikisha malengo yao waliyoyaweka tangu kuanza kwa msimu wa ligi.

Mmoja wa wachezaji walipiga hatua ni kiungo wa Mwadui, Awesu Awesu na kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda ambao wote msimu uliopita walikuwa timu ya Madini SCc ya jijini hapa inayoshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL).

Wawili hao wamekomaa na kufanikiwa kuwa kwenye kiwango cha kuvutia.

 

AWESU AWESU

Kiungo huyo maarufu kama Rasta, ni mmoja wa viungo vijana ambao wana uwezo mkubwa kwa sasa hasa kwenye ligi ya Bongo, wakati akiwa Madini kila mara alieleza lengo lake ni kucheza Ligi Kuu jambo ambalo amefanikiwa kwa asilimia zote.

 Kwenye mchezo wa Kombe la FA mwaka jana dhidi ya Simba, Awesu aliwaburuza viungo wa Simba, hakuna cha Kichuya, Ajibu wala Ndemla walioonekana kwa dakika zote za mchezo zaidi ya Awesu aliyekuwa akizunguka kila kona.

Simba ilionyesha nia ya kumsajili, lakini baadaye ilibadilisha maamuzi na kuamua kumchukua staa wa Yanga, Haruna Niyonzima.

HAKUFA MOYO

Pamoja na kugonga mwamba kutua Msimbazi, Awesu hakukata tamaa aliendelea kuvumilia na kufanya mazoezi muda wote na hatimaye akafanikiwa kutua Mwadui huku michezo ya VPL ya awali akianzia benchi.

“Hadi hivi sasa ligi inavyoelekea ukingoni michezo saba pekee ndio sijacheza na nimefanikiwa kufunga mabao mawili. Moja nilifunga dhidi ya Njombe Mji na jingine dhidi ya Singida United na kwenye FA pia nilifunga dhidi ya Dodoma FC,” anasema Awesu ambaye Januari alichaguliwa kuingia kwenye orodha ya nyota watatu wanaowania tuzo ya mwezi huo.

Moja ya mafanikio anayojivunia ni kupata uzoefu wa kukutana na wachezaji mbalimbali na kumpa nafasi ya kuitwa kwenye timu ya Vijana ya Taifa huku tayari tetezi zinaonyesha msimu ujao huenda akatua kwenye kikosi cha Singida United.

“Kila mchezaji ana ndoto ya kufika mbali kwenye soka hasa kucheza timu kubwa kama vile Simba, Azam, Yanga na hata Mtibwa, hivyo hata mimi ukisikia nimesajiliwa na Simba itakuwa ni maendeleo pia,” Alisema Awesu.

ALIKOTOKEA

Awesu ni mzaliwa wa Zanzibar, alianza soka katika timu ya Arizona iliyopo Visiwani humo kisha kwenda Azam FC kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye kikosi cha timu ya vijana ya Azam kwa muda wa miaka miwili.

Kisha akaenda kituo cha michezo cha Makumbusho kilichopo Dar es Salaam japo hapo hakukaa sana. Juni 2016 ulikuwa mwaka mzuri kwake baada ya kupata shavu Madini Sc kabla ya kwenda Mwadui.

 

RAMADHAN CHALAMANDA

Kwa upande wake Kipa Chalamanda amecheza michezo minne tu tangu atue Kagera, naye amekuwa miongoni mwa nyota wachache waliotoka moja kwa moja SDL hadi Ligi Kuu.

Kipa huyo anasema licha ya kucheza michezo michache, uwepo wa mkongwe, Juma Kaseja kila mara langoni umekuwa darasa tosha kwake.

“Katika michezo minne, miwili ilikuwa mzunguko wa kwanza na mingine mzunguko huu wa mwisho na nilifanikiwa kudaka mchezo dhidi ya Majimaji ambao tulishinda bao 1-0, nikafungwa mchezo mmoja mabao 3-0 dhidi ya Yanga na kutoa sare mbili dhidi ya Azam na Singida United,” anaeleza.

Chalamanda anaeleza kujituma, uvumilivu ndio silaha pekee aliyobaki nayo ya kuhakikisha anapata nafasi zaidi msimu ujao wa ligi katika timu yoyote atakayokuwa nayo.

 

AJIVUNIA KASEJA

Chalamanda anasisitiza kuwepo kwa Juma Kaseja ndani ya Kagera imekuwa bahati ya pekee katika maisha yake ya soka kutokana na anavyomwelekeza vitu anavyopaswa kuwa navyo na kufanya anapokuwa kwenye mchezo.

“Amenieleza vitu vingi ikiwemo kuheshimu kazi yangu na kutakiwa kufanya yale yote ninayotakiwa kufanya ili kufikia malengo bila kutazama changamoto zinazonikabili na tangu nitue hapa tunaishi maisha ya furaha sana,” anasema.

Chalamanda alisaini mkataba wa mwaka mmoja pekee katika timu hiyo hivyo kumalizika kwa msimu kunampa fursa ya kuangalia ustarabu mwingine wa kufanikisha ndoto yake.

 

ALIPOANZIA SOKA LAKE

Chipukizi huyo hana muda mrefu tangu alipoanza kucheza soka kwani alianza kuonyesha kipaji chake akiwa na timu ya Mtwara Kids mwaka 2012 iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Nne aliyodumu nayo kwa muda wa miaka mitatu.

Mwaka 2016 alijiunga na timu ya Namungo FF ya Lindi ambayo alifanikiwa kuipandisha SDL na hapo milango ikafunguka alipotua Madini SC iliyokuwa nayo SDL na baada ya kufanya vyema na kutua Kagera Sugar.