Simba, Yanga kucheza na Everton England

Dar es Salaam: Simba na Yanga na miongoni mwa timu nane ambazo zitachuana kusaka bingwa wa mashindano ya SportPesa Super Cup 2018  yatakayoanza kutimua vumbi Juni 3 hadi Juni 10 nchini Kenya ambapo bingwa ataondoka na kitita cha dola 30,000 ambazo ni zaidi ya Sh 68 mil.

Katika mashindano hayo yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Moi uliopo Kasarani nchini Kenya,  Tanzania itawakilishwa na timu za Simba, Yanga, Singida United na JKU na Kenya ikiwakilishwa na timu nne za huko.

Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa SportPesa Tanzania, Abass Tarimba amesema mbali na kitita hicho cha dola 30,000 kwa timu itakayotwaa ubingwa, timu hiyo pia itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki na Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

"Kuna uwezekano mkubwa mchezo huo na Everton ukachezwa England, hivyo timu itakayotwaa ubingwa wa Sportpesa Super Cup itakwenda Engaland na safari hiyo itagharamiwa na Sportpesa," amesema Tarimba.

Msimu uliopita mashindano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam na Gor Mahia ya Kenya ilitwaa ubingwa na kupata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki na Everton mchezo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mshindi wa pili wa mashindano hayo ataondoka na kitita cha dola 10,000 (Sh 23 mil)  wa tatu atapata dola 7500 (Sh 17 mil) na wanne ataondoka na dola 5000 (Sh 11 mil)  huku timu zote shiriki zikipewa dola 2500 ( Sh 6 mil) kila moja kwa ajili ya maandalizi.