Mbao FC kujiuliza kwa Njombe Mji

Tuesday April 10 2018

 

By Masoud Masasi

Mwanza. Ni vita ya vibonde wa Ligi Kuu, Mbao FC na Njombe Mji  kesho Jumatano zitaonyeshana kazi katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kirumba, Dar es Salaam.

Mbao FC wana pointi 20, wakiwa katika nafasi ya 14 huku Njombe Mji wakiwa na alama 18 na wakishika nafasi ya 15 kwenye Msimamo wa Ligi.

Mchezo huo utakuwa mgumu kwani Mbao FC wanahitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutoshuka daraja msimu ujao.

Njombe Mji nao watakuwa na kibarua kizito katika mpambano huo kwani wakipoteza mchezo huo basi watakuwa wamejiweka kwenye mazingira mabaya ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ettiene Ndayiragije alisema kikosi chake kipo fiti kuwavaa Njombe Mji katika mpambano huo ni muhimu kwao kuweza kupata ushindi.

“Kikosi kipo fiti kuwavaa Njombe Mji huu mchezo ni kama fainali kwetu kwani ni muhimu kupata pointi tatu,” alisema Ndayiragije.

Ndayiragije aliwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa kamwe Mbao FC hawawezi kushuka Ligi Kuu msimu ujao licha ya kutokuwa na matokeo mazuri.