Mourinho atoa sababu ya kipigo cha Man U

Muktasari:

Man City imeweka rekodi ya kushinda mechi 14 za Ligi Kuu kati ya 15

London, England. Licha ya kukata tamaa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, Jose Mourinho amedai wapinzani wao walibebwa katika mchezo wa jana usiku.

Manchester United ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Old Trafford ilichapwa mabao 2-1 na Manchester City katika ‘derby’ iliyokuwa ikisuburiwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani.

Pia, Mourinho amewatwisha mzigo wa lawama mabeki wake akidai waliruhusu mabao ya kizembe. David Silva na Nicolas Otamendi walifunga mabao hayo.

Mourinho alisema Man City ilibebwa na mwamuzi aliyedai alikuwa akitoa uamuzi wa kuipendelea timu hiyo na kuiminya Man United.

Kocha huyo alitoa mfano kwa timu yake kunyimwa mkwaju wa penalti akidai kiungo Ander Herrera alichezewa faulo ndani ya eneo la hatari na Otamendi dakika ya 79.

Herrera alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi kutokana na tukio hilo kwa madai ya kujirusha kutaka mkwaju wa adhabu.

Man City imejiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa baada ya kushinda mechi 14 mfululizo ikiwa kileleni kwa pointi 46 ikifuatiwa na Man United yenye pointi 35.

“Nadhani walikuwa na bahati, bila shaka uamuzi wote ulikuwa wa kutaka kuwabeba. Unatarajia City itafunga mabao mazuri lakini siyo mabao mawili ya kulaumiwa,” alisema Mourinho.

Kocha wa Man City Pep Guardiola alisema walicheza vyema katika idara zote na walistahili kupata ushindi katika mchezo huo.