Simba mtegoni kwa Manula, Okwi

Muktasari:

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wana pointi 58 na mabao 55 na Jumamosi watashuka dimbani kuvaana na Lipuli huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

SIMBA imeanza kunusa harufu ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na sasa wamezidi kuwa moto kwelikweli, na tayari wameweka kambi pale mjini Morogoro kujiwinda dhidi ya Lipuli FC ya Iringa.

Vinara hao wa Ligi Kuu Bara wana pointi 58 na mabao 55 na Jumamosi watashuka dimbani kuvaana na Lipuli huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Lakini Wekundu hao wa Msimbazi kuna mtego wameweka na mahasimu wao, Yanga na kama wakishindwa kucheza karata zao vizuri basi itakula kwao mapema.

Kiungo wa Simba, Jonas Mkude atakosekana kwenye mechi hiyo na Lipuli kutokana na kuwa na kadi tatu za njano, lakini hiyo sio ishu ya kushtua sana unaweza kuipotezea.

Ishu hapa ni kipa tegemeo wa Simba, Aishi Manula na kinara wa mabao Emmanuel Okwi, ambao wana kadi mbili za njano kila mmoja. Sasa mtego ni kwamba, kama Okwi na Manula watacheza dhidi ya Lipuli na ikitokea mmoja wapo tapewa kadi ya njano basi ni dhahiri ataukosa mchezo dhidi ya Yanga. Simba na Yanga zitavaana Aprili 29, mchezo ambao unaweza kuamua nani ataondoka na ubingwa msimu huu.

Hata hivyo, Meneja wa Simba Richard Robart ‘Msomi’, ambaye ndiye anahusika na kutunza kumbukumbu zote za timu hiyo, ameshashtukia mchezo na kuwatonya benchi la ufundi ambao ndio watakuwa na jukumu la kuamua kuwatumia ama la.

Alisema anatambua umuhimu wa mechi na Yanga ambayo inaweza kuwasafishia njia zaidi ya kubeba ubingwa, hivyo anafahamu kila kinachoendelea.

“Mechi na Lipuli ni muhimu na tunahitaji pointi tatu ili kuendelea kusafisha njia ya ubingwa, Manula na Okwi wanaweza wasicheze kwa kuwa kikosi chetu ni kipana,” alisema Mwana.

Kocha msaidizi wa Simba Masoud Djuma alisema wana kikosi kipana na wachezaji wengi ambao, katika kila eneo wapo zaidi ya wawili hivyo wanaweza kushindana bila kuona upungufu wowote.

“Tutangalia mazingira ya mechi na Lipuli, tunaweza kuwatumia Okwi na Manula lakini pia tunaweza kuwapumzisha na nafasi zao wakacheza wengine,” alisema Djuma.

Kama Okwi hatatumika katika mechi hiyo nafasi yake anaweza kuanza Said Ndemla huku Manula akimpisha Said Mohammed ‘Nduda’, ambaye hajacheza tangu asajiliwe kutoka Mtibwa Sugar.

NIYONZIMA APIGWA CHINI

Kiungo fundi wa mpira, Haruna Niyonzima amepigwa chini na Mfaransa Pierre Lechantre kwenye kikosi cha wachezaji 20 waliosafiri jana kwenda Iringa.

Niyonzima, ambaye alitua Simba kwa mbwembwe akitokea Yanga, ameshindwa kuonesha kiwango chake kama ilivyotarajiwa kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Lechantre alisema kuwa, hataweza kumtumia kiungo huyo kutokana na kusumbuliwa na majeruhi hivyo, hatakuwa fiti kwa mapambano.

“Haruna ni mchezaji mzuri, lakini hata katika mechi na Mbeya City nilishindwa kumtumia kwa sababu hukuwa fiti, ametoka katika majeruhi hivyo anahitaji muda wa kupata mazoezi ya ufiti ili kurudi vizuri uwanjani,” alisema Lechantre.