Rachier: Kuondoka kwa Fantoni ni pigo

Muktasari:

Gor Mahia ndiyo timu pekee Kenya inayowakilisha nchi katika mechi za Kombe la Shirikisho la Afrika, watakutana na Yanga ya Tanzania, kwenye mechi ya tatu ya kundi D.

Nairobi. Kuondoka kwa kocha wa viungo, Sandro Fantoni ni pigo kubwa kwa mabingwa wa soka Kenya, klabu ya Gor Mahia.

Muitaliano huyo alibwaga manyanga hivi karibuni na sasa kutokana na ratiba ngumu inayowakabili, Kogalo italazimika kumtafuta mtu wa kuchukua mikoba vinginevyo jahazi lao litazama hasa katika mechi za kimataifa.

Akizungumza na Mtandao rasmi wa klabu hiyo, kuhusu maandalizi ya klabu hiyo pamoja na muelekeo wao katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier, amesema ratiba ngumu inayowakabili inawafanya wachezaji kuchoka na kukosa kocha wa viungo, ni hatari kwao.

Gor Mahia ndiyo timu pekee Kenya inayowakilisha nchi katika mechi za Kombe la Shirikisho la Afrika, watakutana na Yanga ya Tanzania, kwenye mechi ya tatu ya kundi D.

Lakini pia, wana kibarua kingine cha Kombe la Sportpesa Super Cup litakalochezwa mapema mwezi Juni, pamoja na kampeni za kutetea ubingwa wao wa KPL, msimu huu.

“Ukiangalia ratiba yetu, utagundua kuna kazi kubwa ya kufanya. Tuna zaidi ya mechi 50, msimu huu, hii inahitaji akili na mwili iliyotulia na yenye utayari mkubwa. Hivyo basi, baada ya kuondoka kwa Santoni, tunalazimika kutafuta mtu makini wa kufanya kazi aliyokuwa anaifanya," amesema Rachier.

Kwa mujibu wa Rachier, klabu imeshatoa tangazo kwenye mtandao wao, mwisho wa kutuma maombi ni leo mchana na  yanatumwa kwenye anuani yao.