Eti kocha Allegri kachomoa kwenda Arsenal

Tuesday May 15 2018

 

TURIN, ITALIA

KOCHA Massimiliano Allegri amegomea nafasi ya kwenda kurithi mikoba ya Arsene Wenger huko Arsenal baada ya kudai ataendelea kuinoa Juventus msimu ujao.

Tangu Wenger alipotangaza mpango wa kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu, Allegri amekuwa mmoja kati ya majina ya makocha maarufu wanaopewa nafasi ya kwenda kuinoa timu hiyo yenye maskani yake Emirates.

Lakini baada ya kuisaidia Juventus kubeba ubingwa wake wa saba mfululizo wa Ligi Kuu Italia ‘Serie A’, Allegri alisema mpango wake ni kuweka mambo sawa na kutengeneza kikosi matata cha Wataliano hao kiwe tayari kwa mikikimikiki ya msimu ujao.

Alisema: “Kama hawatanifukuza, nadhani nitaendelea kubaki Juventus hata mwakani pia.

“Sina uhakika kuhusu mambo ya baadaye, hilo linahusu mipango ya Juventus itakavyokuwa. Nadhani baada ya kumaliza hivi kwa kushangilia, tutakaa chini na kuweka mipango sawa.Msimu ujao ukianza, tutaanzia na pointi sifuri na kuona kile tutakachokifanya kuboresha ubora kwenye ushindani.”

Allegri pia amekuwa akihusishwa kwenye mpango wa kuwa kocha wa Chelsea, huku timu hizo mbili za London zote zikishindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.