Cheki hizi rekodi za wapinzani wa Yanga

Muktasari:

  • Kuanzia hatua ya makundi na zinazofuata, Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hutoa mgawo wa fedha kwa klabu ambazo zimeingia kwenye kila hatua ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake.

FEDHA ziko mdomoni mwa wawakilishi wa Tanzania, Yanga iwapo itakaza msuli katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufuzu hatua zitakazofuata za mashindano hayo.

Kuanzia hatua ya makundi na zinazofuata, Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hutoa mgawo wa fedha kwa klabu ambazo zimeingia kwenye kila hatua ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake.

Ukitazama ubora, viwango na mafanikio ambayo timu 16 zilizofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho zinazo, ni wazi Kundi D ambalo Yanga ipo pamoja na USM Alger ya Algeria, Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sports ya Rwanda, linaonekana sio gumu kwa wawakilishi hao wa Tanzania

Gazeti hili linakuletea baadhi ya taarifa muhimu zinazohusu timu ya Gor Mahia ya Kenya ambayo, ni miongoni mwa wapinzani wa Yanga kwenye hatua hiyo ya makundi.

Historia yake

Gor Mahia ilianzishwa rasmi Februari 17, 1968 ikibadili jina kutoka Luo Union ambayo chimbuko lake lilikuwa ni miaka ya 1920.

Inatajwa kama moja ya timu kubwa, kongwe na zenye mashabiki wengi sambamba na mafanikio makubwa nchini humo ikiwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya mara 16 ambazo ni nyingi zaidi kuliko timu nyingine huku ikiwa imetwaa Kombe la FA Kenya mara 10

Ina rekodi nzuri katika mashindano ya klabu Afrika kwani ndio timu pekee ya Afrika Mashariki na Kati iliyowahi kuchukua ubingwa wa Afrika kwa ngazi ya klabu ikiwa imetwaa Kombe la Washindi mwaka 1987.

Kufuzu kwake kwenye hatua hiyo kumeifanya iweke rekodi ya kuwa timu pekee ya Kenya iliyowahi kuingia hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu.

Imekuwa ikiungwa mkono na kundi kubwa la raia wa Kenya na kwa kuthibitisha hilo, miongoni mwa viongozi wa awali walikuwa ni Wanasiasa, Tom Mboya na Jaramongi Oginga Odinga.

Kocha Mkuu

Gor Mahia inanolewa na Kocha Muingereza, Dylan Kerr, ambaye kabla ya kujiunga nayo alikuwa akiinoa Simba ya Tanzania katika msimu wa 2015/2016.

Hata hivyo, Kerr hakumaliza msimu huo kwani alidumu kwa miezi sita tu baada ya mkataba wake kuvunjwa kutokana na timu hiyo kufanya vibaya kwenye Kombe la Mapinduzi, Januari mwaka 2016.

Akiwa na Simba alikutana na Yanga mara moja na kupoteza kwa mabao 2-0 hivyo, kukutana nayo tena itakuwa kama ni fursa kwake kutafuta namna ya kulipa kisasi.

Hata hivyo, kocha huyo alisema kundi hilo sio la kubeza na inahitajika kupambana ili kusonga mbele.

“Ni kundi gumu na naamini sio kwetu tu, bali kwa timu zote nikianzia na Yanga, USM Alger na Rayon Sports. Kwanza sina taarifa zozote muhimu kuhusu wapinzani wetu, lakini nitazipata na kuzifanyia kazi kwa haraka.”

Mastaa muhimu

Silaha kubwa ya Gor Mahia ama Kogalo ni kipa Bonifas Oluoch, ambaye amekuwa muhimili imara wa timu hiyo katika safu ya ulinzi. Pia, wapo kina Godffrey ‘Jaja Walu’ Walusimbi, Haruna Shakava na nahodha Musa Mohammed. Hapo mbele wana Mnyarwanda, Jacq Tuyisenge, Meddie Kagere na George Odhiambo ‘Blackberry.

Rekodi Yanga vs Gor Mahia

Mara ya mwisho kwa Yanga kukutana na Gor Mahia ilikuwa ni mwaka 2015 kwenye mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) ambapo Yanga ilipoteza kwa mabao 2-1.

USM Alger

Rekodi zinaonyesha ni timu tamu kwelikweli na kuna mastaa watatu, ambao Yanga inabidi kuwachunga sana.

Kuna Farouk Chafaп, ambaye ni beki wa nguvu na washambuliaji matata wa Yanga, Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa watakuwa na kazi naye.

Pia, kuna Faouzi Yaya na kinara wa mabao, Oussama Darfalou ambaye ni straika wa kati na anasumbua kwelikweli akiwa na mabao 14 mpaka sasa.

Union Sportive de la mйdina d’Alger ama USM Alger, makao yake makuu yapo katikati ya Jiji la Algeria na ilianzishwa mwaka 1937.

Uwanja wake wa nyumbani ni Omar Hamadi Stadium wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 12,000 kwa wakati mmoja.

USM Alger ni miongoni mwa timu zenye mafanikio katika soka la Algeria ikibeba ubingwa mara 17 na Kombe la Ligi mara nane.

Mafanikio makubwa kwa timu ya USM Alger katika michuano ya kimataifa ni kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na kupoteza mbele ya TP Mazembe.

RAYON SPORT

Rayon Sport ilianzishwa Mei 1968, makao makuu ya klabu hiyo yapo Kigali, Rwanda na uwanja wake wa nyumbani ni Amahoro ambao una uwezo wa kubeba mashabiki waliokaa 25,000.

Benchi la ufundi la Rayon Sport linaongozwa na Kocha Mkuu, Ivan Minaertn akisaidiana na Djano Witakenge pamoja na kocha wa makipa, Nkunzingoma Ramadhani.

Rayon Sport ina mafanikio kuanzia katika ligi ya ndani ikiwa imechukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda mara nane. Imechukua Kombe la cha Ligi mara tisa na kuchukua ubingwa wa Cecafa mara moja mwaka 1998.

Uzoefu wake katika Kombe la Shirikisho ukiweka mbali msimu huu, iliwahi kuishia katika hatua ya awali mwaka 2006 na 2008, na baada ya hapo ilishindwa kupata nafasi ya kucheza mashindano hayo hadi mwaka 2017, ilipoishia hatua ya pili.

Rayon ina wachezaji watatu wa kuchungwa ambao ni washambuliaji, Muhire Kevin na Nahimana Shassir ambaye aliifunga Azam mabao mawili katika mechi ya kirafiki mwanzoni mwa msimu baadaye alihusishwa kujiunga na Simba.

Nyota mwingine ambaye Yanga inatakiwa kumchunga ni kiungo, Pierre Kwizera ambaye ameshawahi kuicheza Simba dhidi ya vigogo hao wa Tanzania.

Rayon Sport ipo katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Rwanda ikiwa na pointi 30, imecheza mechi 15, imeshinda tisa, imetoka sare tatu, imefungwa tatu, imepchika mabao 29, ikifungwa tisa na inawastani ya mabao 12.

Timu inayoongoza Ligi Kuu ya Rwanda ni APR yenye pointi 34, lakini ipo mbele kwa mechi mbili dhidi ya Rayon Sport ikiwa imecheza michezo 17.