Usajili Yanga waingiliwa kati

MABOSI wa usajili wa Yanga, jana Jumapili walikutana kwenye hoteli moja ya kitalii jijini Dar es Salaam ili kupanga mikakati ya kufanya usajili wa maana kwa maandalizi ya mechi zao Kombe la Shirikisho Afrika na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, huku nyuma nyota wa timu hiyo na wadau wa klabu hiyo wameamua kutoa ushauri wao wakitaka usajili huo ufanywe kwa umakini na hasa eneo la ushambuliaji kwa kuhakikisha straika wanayemnasa awe na sifa kuu mbili, upambanaji na ufungaji.

Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyesaidia Yanga kuwanasa Malimi Busungu kutoka Mgambo JKT na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alisema, kikosi chao kina tatizo eneo la mbele hivyo mabosi wa usajili lazima wahakikishe wanarekebisha hilo kuliko eneo jingine.

“Safu ya mbele lazima apatikane mchezaji atakayeamua mechi iwe kipindi ambacho Yanga ipo vizuri ama kuzidiwa, nadhani hapo panahitaji umakini zaidi,” alisema.

Naye Emmanuel Martin alisema: “Tunapaswa kuwa na watu wa kazi mbele kama ilivyo kwa watani zetu wa Simba walio na John Bocco na Emmanuel Okwi ambao wamekuwa wakifanya maamuzi katika mechi tofauti na kupelekea kuwa mabingwa kwa msimu ulioisha.”

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alifafanua kitaalamu zaidi kuhusiana na usajili kufanywa kwa mahitaji ya kocha Zahera Mwinyi, kwamba hata kama hajapata muda mwingi wa kuangalia ligi aangalie mikanda ya wachezaji wa timu kujua madhaifu.

“Yanga inahitaji marekebisho makubwa, kocha anaweza akaangalia baadhi ya mechi walizocheza wachezaji wa Yanga, lazima atabaini ni safu gani inahitaji marekebisho makubwa zaidi.

“Binafsi naona safu ya ushambuliaji inahitaji mtu mwenye akili nyingi, nguvu, mfungaji na mpambanaji na anayejua Yanga inahitaji kitu gani na sio wa kujaribishwa, hicho ndicho kiliwasumbua Simba walivyompata Okwi na Bocco, tatizo limeisha,” alisema.

Hata hivyo winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe, alisema licha ya kuwa mpinzani wa Yanga, lakini kwa maendeleo ya soka nchini na ushindani, Wana Jangwani hao wanahitaji kumpata mshambuliaji asiye mbabaishaji.

“Wasikurupuke kusajili, wajaribu kutenga muda wa kupata wanaume wa kazi kama walivyofanya kwa kwa Papy Kabamba Tshishimbi, Thabani Kamusoko au Donald Ngoma kwani itasaidia kuwarejesha katika ubora wao,” alisema Ulimboka.