Singida United haiachi kitu

SINGIDA United haitanii kabisa katika suala la usajili na kwa kudhihirisha hilo imefanikiwa kumsainisha mshambuliaji wa Prisons, Eliuter Mpepo, ambaye anakuwa mchezaji mpya wa tano kujiunga na timu hiyo siku chache tu baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara.

Washindi hao wa pili wa Kombe la FA wamepata pigo la kuondokewa na nyota kadhaa kama Tafadzwa Kutinyu na Mudathir Yahaya ambao wote wawili wamekwenda Azam wakimfaata kocha wao Hans Pluijm ambaye naye alishaanzasha safari ya kujiunga na timu hiyo.

Mpaka sasa wababe hao kutoka mji maarufu kwa mafuta ya Alizeti, wamewasainisha nyota wapya watano ambao ni Amara Diaby kutoka Asec Mimosas na Kazungu Mashauri kutokea Tanzania Prisons.

Wengine ni washambuliaji Habibu Haji Kyombo (Mbao FC), Tiba John (Ndanda) na jana Jumapili walimtambulisha Mpepo ambaye katika ligi ya msimu uliopita, alifunga mabao matano na kuwa miongoni mwa washambuliaji waliofanya vizuri na kikosi cha Prisons ya Mbeya.