#WC2018:Manchester derby itapigwa Russia 2018

MAMBO yanazidi kunoga. Kila mmoja ameshafahamu anakwenda kukutana na nani kwenye fainali hizo matata kabisa za huko Russia na hivi ndivyo itakavyokuwa vita ya kwenye Kundi F.

KUNDI F

Timu zinazounda kundi:
Ujerumani
Mexico
Sweden
Korea Kusini

Utamu kamili
Kama utapewa nafasi ya kutabiri bingwa wa Kombe la Dunia 2018 basi kamwe usiwaweke kando Ujerumani. Wababe hao wa Ulaya watakwenda kwenye fainali hizo za Russia wakiwa mabingwa watetezi baada ya kuibuka na ubingwa miaka minne iliyopita huko Brazil walipoichapa Argentina ya Lionel Messi katika mchezo wa fainali. Bila ya shaka, Ujerumani itakwenda kwenye fainali hizo kikosi chake kikiwa na mchanganyiko wa mastaa wale wenye uzoefu na ambao makinda. Kwa upande wa makinda kuna mastaa kama Leroy Sane, Timo Werner na Julian Draxler, lakini kwenye bakuli la wenye uzoefu, utakuta majina ya viungo makini kama Toni Kroos na Mesut Ozil. Lakini, Ujerumani ina mtihani mzito kwenye fainali hizo kutokana na kupangwa kwenye kundi lenye upinzani mkali kwa kuwa na timu zenye mastaa wa maana kwenye vikosi vyao. Wamepangwa na Sweden, ambao wanaweza kumjumuisha Zlatan Ibrahimovic, lakini wapi pia na Mexico ya Javier Hernandez maarufu kama Chicharito na Korea Kusini ya fundi wa mpira wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min. Sweden pia itakuwa na huduma ya beki wa kati wa Man United, Victor Lindelof, hivyo kufanya kundi hilo kuwa na mastaa wanaotambulika, lakini watakafanyaa Manchester derby ipigwe Russia kwa maana ya Sane na Lindelof.

Ratiba ya Kundi F
Jumapili, Juni 17 - Germany vs Mexico, Moscow
Jumatatu, Juni 18 - Sweden vs Korea Kusini, Nizhny Novgorod
Jumamosi, Juni 23 - Korea Kusini vs Mexico, Rostov-on-Don
Jumamosi, Juni 23 - Ujerumani vs Sweden, Sochi
Jumatano, Juni 27 - Korea Kusini vs Ujerumani, Kazan
Jumatano, Juni 27 - Mexico vs Sweden, Yekaterinburg