Banda yeye ni bata kwa kwenda mbele

BEKI wa Baroka FC iliyopo Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL), Abdi Banda, yupo nchini akiendelea na mapumziko yake baada ya kumaliza mechi za ligi hiyo, sasa unaambiwa nyota huyo hataki kabisa kusikia habari za mpira.

Juzi kati beki huyo kiraka, alikuwa Zanzibar akila bata na mchumba wake Zabibu Kiba na mwanaye aitwaye Kassim. Unaambiwa huko ilikuwa kujipa raha tu.

Meneja wa mchezaji huyo wa zamani wa Simba, Abdul Ahmed ‘Bosnia’ amesema Banda yupo nchini akila bata ambapo ratiba yake inamtaka apumzike kabisa na akili yake isiwe na mambo yanayohusiana na mpira, hali ambayo imekuwa tofauti na miaka ya nyuma kwa mchezaji huyo.

“Hatakiwi kujihusisha na masuala ya mpira katika kipindi hiki. Anatakiwa afanye mazoezi mepesi kidogo na Gym. Kama ulimwangalia katika mechi ya Ali Kiba na Samatta hakuwa kama siku zote,” alisema.

“Programu ambazo anawekewa na klabu yake ni kuhakikisha anakuwa vizuri na anapumzika kwa sababu ameichezea timu yake takribani asilimia 90, hivyo ameambiwa apumzike kwa wingi ili akirejea huko awe katika kiwango kile kile.”

Akizungumzia taarifa za mchezaji wake kuhusishwa kutimkia barani Ulaya, alisema kwamba ofa zipo na alikuwa akizungumza na mawakala wenzake hivyo mambo yakiwa tayari wataweka wazi.

Naye Banda alililimbia Mwanaspoti akisema: “Nilienda Zanzibar kutembea tu, si unajua baada ya kazi wakati mwingine unatakiwa kuondoa ‘stresi’ ili unaporudi kazini uwe na akili na nguvu mpya.”

Alisema katika matembezi yake hayo, alienda katika fukwe mbalimbali na pia kutembelea vivutio mbalimbali vya utali

“Kwa sababu ni kufurahi tu hivyo nilitembea sehemu mbalimbali kwa ajili ya kujifunza na kuweka sawa akili nilikwenda mpaka kule kwenye mbuga zao zile ndogo ndogo za wanyama,” alisema.