#WC2018: Hebu ona hii timu ya fainali

Muktasari:

  • Sasa, hebu angalia itakuwa vipi kama utatengeneza kikosi cha 'First XI', nchi gani itakuwa na wachezaji wengi? Kwa kuangalia kiwango cha mchezaji kwenye fainali hizi, hebu angalia.

Ufaransa na Croatia zimeingia fainali ya Kombe la Dunia na tayari majina makubwa yamejitokeza. Kylian Mbappe, Luka Modric, Antoine Griezmann na Mario Mandzukic wamezibeba timu zao kiasi cha kuzipeleka fainali.
Sasa, hebu angalia itakuwa vipi kama utatengeneza kikosi cha 'First XI', nchi gani itakuwa na wachezaji wengi? Kwa kuangalia kiwango cha mchezaji kwenye fainali hizi, hebu angalia.
 Kipa – Hugo Lloris: Ni kipa mwenye uwezo mkubwa. Huenda akawa kipa bora wa fainali za mwaka huu Russia, aliokoa michomo ya ajabu dhidi ya Uruguay na Ubelgiji na kuisaidia Les Blues kutinga fainali.
Fulubeki wa kulia – Sime Vrsaljko: Beki wa Atletico Madrid alicheza mpira mkubwa mechi dhidi ya England licha ya kuwa alikuwa majeruhi.
Beki wa kati – Raphael Varane: Aliibeba Ufaransa na kufanya vizuri mechi ya robo fainali dhidi ya Uruguay na uwezo wake wa kusimama kati umeisaidia timu yake kufanya vyema. Unaweza kusema ndiye beki bora wa kati duniani kwa sasa.
Beki wa kati – Domagoj Vida ameonyesha kiwango. Unaweza kumtaka kama mmoja wa mabeki bora katika fainali za mwaka huu.
Fulubeki wa kushoto – Ivan Strinic: Anatambua anachokifanya uwanjani. Ni mmoja kati ya mabeki matata. Ana uwezo mkubwa kwa kile anachokifanya uwanjani.

Alionyesha mambo makubwa kiasi cha kukaribia kupasuka mapafu katika mechi za Russia na  England akiwatuliza Mario Fernandes na Kieran Trippier.
Kiungo wa kati – N’Golo Kante: Mashine ya Chelsea ameonyesha mpira mkubwa sana katika fainali za mwaka huu. Ameisaidia pakubwa Ufaransa katika fainali hizi.
Kiungo wa Kati – Luka Modric: Anawania Tuso ya mchezaji bora kama ilivyo kwa Kante. Modric amekuwa mtu wa kubadilisha matokeo inapokuja dakika 120.

Kiungo wa kati – Ivan Rakitic: nyota wa Barcelona alikuwa msaada mkubwa kwa Croatia katika fainali za mwaka huu. Ana uwezo mkubwa wa kubadili mchezo mazingira yanapokuwa magumu.
Wingi ya kulia – Kylian Mbappe: ni hazina ya Ufaransa waliokuwa nayo katika fainali za mwaka huu, Mbappe ameisaidia pakubwa Ufaransa. Alifunga mabao mawili muhimu dhidi ya Argentina pia alichangia na Ubelgiji.
Mshambuliaji – Mario Mandzukic: Huyu ana upekee anapokuwa uwanjani. Amejitolea kwa Croatia katika hatua ya mtoano dhidi ya England.
Wingi ya kushoto - Ivan Perisic –Hakuwa na wakati mzuri katika fainali za mwaka huu, lakini alikuwa na mchango muhimu katika kikosi cha Croatia. Amekuwa tishio anapokuwa akikokota mpira.