#WC2018: Rekodi za Ronaldo alizoweka 2018

KAMA kuna mtu mwenye kismati tangu mwaka huu wa 2018 ulipoanza, basi ni supastaa wa Ureno na Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

Kwa sasa staa huyo wa zamani wa Manchester United anafanya mambo yake matamu huko Russia kwenye fainali za Kombe la Dunia ambako tayari ameshaweka rekodi kadhaa.

Wakati ukiendelea kumfurahia Ronaldo na makali yake kwenye soka, hizi hapa ni rekodi ambazo staa huyo ameziweka katika mwaka huu wa 2018.

9. Afunga bao moja katika friikii 45

Ronaldo ni mfano halisi kwamba mtu hupaswi kukata tamaa. Katika maisha yake ya soka la kimataifa, staa huyo wa Ureno alijaribu mara 44 kupiga mipira ya adhabu, lakini hakuweza kushinda kwenye michuano ya Euro na Kombe la Dunia kabla ya kufanya tena mara yake ya 45 kwenye fainali za huko Russia na kuweka kwenye nyavu.

Hiyo ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Hispania, ambapo alifunga hat-trick katika sare ya 3-3. Siku hiyo Ronaldo alifunga hat trick yake ya 51 na jambo zuri Hiyo pia ilikuwa hat trick ya 51 kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia.

8. Amebeba mara saba Kiatu cha Dhahabu Ulaya

Ronaldo hakufunga bao kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, wakati timu yake ya Real Madrid iliichapa Liverpool, lakini Mreno huyo aliibuka kuwa kinara wa mabao wa michuano hiyo. Ronaldo alifunga mabao 15 katika mechi 13. Hiyo ilikuwa mara yake ya saba kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kunyakua Kiatu cha Dhahabu cha michuano hiyo. Kwa ujumla, Ronaldo amefunga mabao 120 katika michuano hiyo ya Ulaya, akipiga hat-trick mara saba, mabao mawili kwenye mechi moja mara 32, mabao ya friikiki mara 12, fainali amefunga mabao manne, nusu fainali mabao 13, robo fainali mabao 21, kwenye mtoano mabao 60.

7.Kufunga kwenye mechi 11 mfululizo

Ronaldo anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa nyakati zote kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiweka wavuni mara 120. Ronaldo pia ndiye mchezaji aliyewahi kufunga mabao mengi zaidi ndani ya msimu mmoja kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutupia wavuni mara 17.

Supastaa huyo wa Ureno ameweka rekodi pia ya kuwa mchezaji pekee aliyewahi kufunga kwenye mechi 11 mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akiwa mchezaji wa tatu kufikisha mechi 150 kwenye michuano hiyo. Bayern Munich ndiyo iliyomzuia Ronaldo asiendeleze rekodi yake ya kufunga mfululizo, kwani alikumbana nayo ikiwa ni mechi yake ya 12 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa ametokea kufunga mfululizo kwenye mechi 11 zilizopita. Rekodi ya nyuma ilikuwa kufunga kwenye mechi 10 mfululizo.

6.Afunika Ulaya nzima kwa mabao ya kimataifa

Ni hivi, hakuna mchezaji yeyote ndani ya Bara la Ulaya, ndiyo yaani Ulaya nzima aliyefunga mabao mengi kuliko supasta Cristiano Ronaldo.

Staa huyo ametupia mabao 85 kwenye mechi 152. Wakati anaweka rekodi yake ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, kwenye mechi dhidi ya Hispania, hapo Ronaldo alikuwa amefikisha mabao 84, ambayo yalimfanya alingane na gwiji wa Hungary, Ferenc Puskas kwa kufunga mabao kwenye soka la kimataifa. Lakini baada ya hapo, Ronaldo akaongeza bao jingine Ureno ilipocheza na Morocco na hivyo kuwa na mabao 85, ambayo ni mengi kuwahi kufungwa na mchezaji wa taifa la Ulaya kwenye michuano ya kimataifa. Mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye soka la kimataifa, rekodi hiyo inashikiliwa na Ali Daei aliyefunga mara 109 akiwa na kikosi cha Iran.

5. Mabao mengi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ronaldo amesukumia wavuni mabao 120 kwenye mechi 150 na amepiga asisti 40 pia. Kutokana na hilo, staa wa Barcelona na Argentina, Lionel Messi atahitaji kufunga mabao 20 huku akiombea Ronaldo asifunge tena ili kufikia rekodi yake kwenye michuano hiyo ya Ulaya.

Msimu uliopita, Ronaldo alifunga mabao 15 katika mechi 13 na hivyo kumfanya afikishe idadi ya mabao 120 kwenye michuano hiyo. Messi amefunga mabao 100 na staa wa zamani wa Real Madrid, Raul Gonzalez anashika namba tatu na mabao yake 71 na Karim Benzema anashika namba nne kwa kutupia wavuni mabao 56.

4.Ushindi mara nyingi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Kwa mwaka huu, Ronaldo ameweka rekodi ya kuwa kwenye timu ya ushindi mara 97 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Jambo hilo linamfanya Ronaldo kuingia kwenye historia ya kuwa mchezaji ambaye timu yake aliyochezea imeshinda mara nyingi zaidi kwenye michuano hiyo ya Ulaya. Wakati Real Madrid inaichapa Liverpool 3-1 kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huo ulikuwa ushindi wa 97 kwa Ronaldo kati ya mechi 159 alizocheza kwenye michuano hiyo.

Ushindi huo unaweza kufika mechi 100 kama utajumlishwa pia na ule wa mechi za kufuzu kipindi hicho alipokuwa akikipiga Sporting Lisbon.

3.Mchezaji mwenye umri mkubwa kufunga hat-trick Kombe la Dunia

Unaweza kuyachukulia kiwepesi tu yale mabao matatu aliyofunga Cristiano Ronaldo kwenye mechi dhidi ya Hispania katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea huko Russia. Mabao hayo matatu, ambayo siku hiyo Ronaldo alikuwa akikabwa na wachezaji aliowazoea Sergio Ramos na Gerrard Pique yamemfanya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kuwahi kufunga mara tatu ndani ya mechi moja.

Hiyo ni historia, hakuna mchezaji mwenye umri kama wa Ronaldo, ambaye alifunga mabao matatu ndani ya mechi moja ya Kombe la Dunia. Ronaldo ana miaka 33.

2.Mataji mengi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Ronaldo ndiye mchezaji mwenye mafanikio makubwa zaidi kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mreno huyo hakufunga dhidi ya Liverpool walipokutana huko Kiev, Ukraine, lakini timu yake ya Los Blancos imeshinda na kubeba ubingwa ambao umekuwa wa tano kwenye historia ya mchezaji huyo. Sawa, Ronaldo hakufunga kwenye fainali, lakini bila ya mabao yake Real Madrid isingefika fainali yenyewe. Real Madrid amebeba mataji manne akiwa na Real Madrid na taji moja alilibeba akiwa na Manchester United mwaka 2008 kabla ya mwaka mmoja baadaye kwenda kujiunga na Los Blancos.

1.Rekodi ya mabao Kombe la Dunia

Ronaldo alifunga mabao matatu kwenye mechi ya kwanza ya Ureno kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, ambapo mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 3-3 dhidi ya Hispania.

Katika mechi hiyo, Ronaldo alifunga bao lake la kwanza dakika ya nne tu ya mchezo kwa mkwaju wa penalti baada ya yeye mwenyewe kuangushwa ndani ya boksi na Nacho.

Bao hilo lilimfanya Ronaldo kuwa mchezaji wa nne kufunga katika fainali nne tofauti za Kombe la Dunia. Wachezaji wengine waliowahi kufanya hivyo ni Uwe Seeler, Pele na Miroslav Klose. Hakuna mashaka ataendelea kufunga zaidi wakati atakapokwaana na Iran katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi katika kundi lao.