#WC2018: Uvumilivu wawashinda Serbia

Moscow, Russia. Chama cha soka cha Serbia kimeilima barua FIFA kikilalamikia kuwepo maagizo kwa waamuzi kuwapa ushindi wapinzani wao Uswisi, katika mechi yao iliyopigwa Ijumaa iliyopita.
Katika mchezo huo wa kundi E, Serbia waliongoza kwa bao la mapema lililofungwa na Aleksandar Mitrovic dakika ya tano na kudumu hadi mapumziko kabla ya Granit Xhaka kuisawazishia Uswisi dakika ya 52 na Xherdan Shaqir kufunga bao la ushindi dakika ya 90.
Kocha wa Serbia, Slavisa Kokeza alikua wa kwanza kulalamika akisema walicheza na timu iliyoandaliwa kushinda kwani walichezewa viabaya lakini hakuna aliyejali.
“Ninaweza kusema wakati tunacheza mechi ya leo ‘juzi’ tulikua na mpinzani zaidi ya Uswisi, bila shaka FIFA walikua upande wa wapinzani wetu, nadhani kulikua na maagizo maalumu,” alisema.
Alisema alimshangaa kuona VAR haijawasaidia kupata penalti baada ya mwamuzi aliyechezesha mechi yao kutoka Ujerumani kuwanyima penalti licha ya mchezaji wao Aleksandar Mitrovic kuangushwa na wachezaji wawili wa Uswisi karibu kabisa na lango la wapinzani.
Serbia iliyoanza michuano hiyo kwa kuilaza Costa Rica bao 1-0 ilihitaji ushindi katika mchezo huo ili kujihakikishia kutinga hatua ya 16 bora huku ikiwa na mechi mkononi ambapo sasa itabidi ipambane kusaka matokeo itapocheza mechi yake ya mwisho ya makundi dhidi ya Brazil Juni 27.
Mmoja wa maofisa wa FIFA amekiri kuipokea barua hiyo ya malalamiko kutoka Serbia na kusema wanasubiri kupokea vilelezo kama amvayo chama cha soka Serbia kimetakiwa kufanya na kamati husika itaketi haraka iwezekanavyo kuyafanyia kazi malalamiko hayo na kutoa maamuzi.