Ronaldo awavusha Ureno, ataka Paundi 135 mil kwa wiki

HADI kufikia jana Jumatano saa 9:04, Cristiano Ronaldo alikuwa ameshapiga mabao manne kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.

Zile tatu kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Hispania na lile moja la haraka sana aliloipiga Morocco kwenye mechi ya pili kwenye Kundi B. Mechi hiyo iliishia kwa matokeo hayo ambayo yanayoifanya Ureno kutinga hatua ya 16 bora, huku wakiifungisha virago Morocco na kuwa nchi ya kwanza kuaga michuano hiyo. Morocco sasa imebakiza mechi moja tu ya kukamilisha ratiba ambapo watakipiga na Hispania. Ronaldo ameanza kwa moto kwenye fainali hizo ambapo ameonekana wazi kwamba kweli anakitaka Kiatu cha Dhahabu kwenye fainali hizo ambazo miaka minne iliyopita, James Rodriguez alikinyakua huko Brazil.

Ureno sasa inaungana na Russia kutinga hatua ya 16 bora na iliwaacha Hispania ambao jioni ya jana walitarajia kumenyana na Iran katika mechi ambayo ingetoa hatima ya moja ya timu katika kundi hilo kutambua ni ipo itakwenda kuungana na Ronaldo kwenye hatua hiyo ya kibabe kabisa.

Lakini, kwa sasa achana na hilo. Ishu inayoleta mjadala kwa sasa ni kuhusu ripoti kwamba staa huyo wa Ureno anataka kurudi Manchester United. Baada ya kuonyesha makali ya wembe na kutisha kwenye kutikisa nyavu, ambapo mechi mbili bao nne kwenye fainali za Kombe la Dunia, Ronaldo sasa amekuwa habari ya mitaa mbalimbali ya huko Russia wakisema mchezaji huyo ni shinda kutokana na hayo makali aliyoanza nayo.

Ronaldo anaripotiwa kuwanunia mabosi wa Real Madrid kutokana na kumpa mshahara kiduchu, ambao amegundua pia hata Antoine Griezmann mkwanja anaolipwa huko Atletico Madrid ni mkubwa kuliko anaolipwa yeye.

Awali, Ronaldo alikuwa akipambana na waajiri wake huko Bernabeu kutaka wamwongezee mshahara ili kuwafikia Lionel Messi na Neymar, lakini ripoti zilizoibuka hivi karibuni kumbe hata Griezmann analipwa pesa ndefu kuliko yeye, hilo limemkasirisha zaidi.

Ronaldo ameanza kwa kasi kubwa sana kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia na kiwango chake lazima kitawafanya Real Madrid kukubali kukaa mezani kumpa dili jipya, lakini pia linaweza kuwafanya Man United pia kumhitaji kwa sababu wanamini wataendelea kuvuna huduma bora kabisa licha ya umri wake kwa sasa kuwa mkubwa. Ronaldo na umri wa miaka 33.

Gazeti moja la Italia, Libero linaripoti Ronaldo anaweza kuchukua uamuzi wa kurudi Old Trafford baada ya kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Lakini, hilo linaweza kuingiliwa kati na Paris Saint-Germain, ambayo pia imekuwa ikiisaka huduma ya mshambuliaji hiyo licha ya kukabwa na ile sheria ya Uefa kuhusu matumizi kwenye usajili wa wachezaji.

Ronaldo alisema baada ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tu dhidi ya Liverpool anataka kuondoka Bernabeu kwa kubainisha nyakati zake za kuwa hapo zimefika mwisho.

Taarifa za kutoka Bernabeu zilibainisha jambo hilo limewatibua Rais Florentino Perez na wakurugenzi wa bodi kwa sababu amekwenda kutoa maelezo kwenye eneo lisilostahili.

Kwa sasa Ronaldo analipwa mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki, kama anaolipwa Mesut Ozil huko Arsenal, wakati Neymar analipwa Pauni 619,000 kwa wiki huko PSG na Lionel Messi analipwa Pauni 673,000 kila baada ya siku saba.

Kuna taarifa zinadai Ronaldo anataka alipwe mshahara wa Pauni 1.35 milioni kwa wiki kitu ambacho kitakuwa kigumu kukubalika. Kwenye kikosi cha Man United mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi ni Alexis Sanchez, hivyo ujio wa Ronaldo ni wazi unaweza kutikisa tena bili ya mishahara ya timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford. Staa mwingine wa Real Madrid anayehusishwa na mpango wa kutua kwenye kikosi cha Man United ni Gareth Bale, ambaye alifichua hivi karibuni kwamba ataanza kutazama upya hatima yake kwenye kikosi hicho kwa sababu hakimpi nafasi ya kutosha ya kucheza na yeye anataka timu ambayo itamhakikishia nafasi. Kwa muda sasa Ronaldo na Bale wamekuwa wakihusishwa na miamba hiyo ya Man United ambayo kocha Jose Mourinho anajaribu kukijenga kikosi chake kupambana na wapinzani wao wa Manchester City kwenye Ligi Kuu England msimu ujao baada ya kutesa mwaka huu wakimaliza ligi hiyo kwa pointi 100 walizovuna kwenye mechi 38.