#WC2018: Wakata utepe Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Kinachosubiriwa ni kuona ni mchezaji gani atakuwa wa kwanza kufunga kwenye fainali hizi za Russia, atakuwa wa timu wenyeji au atakuwa wa Saudia? Makala haya yanakuletea wachezaji wote waliofunga mabao ya kwanza katika fainali zote za Kombe la Dunia tangu zilipoanza mwaka 1930.

WENYEJI Russia na Saudi Arabia watakata utepe kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 zitakazoanza rasmi Alhamisi ijayo.

Kinachosubiriwa ni kuona ni mchezaji gani atakuwa wa kwanza kufunga kwenye fainali hizi za Russia, atakuwa wa timu wenyeji au atakuwa wa Saudia? Makala haya yanakuletea wachezaji wote waliofunga mabao ya kwanza katika fainali zote za Kombe la Dunia tangu zilipoanza mwaka 1930.

Lucien Laurent, Ufaransa (1930)
Hili ndilo bao la kwanza kufungwa kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia.
Kwenye mechi hii ya ufunguzi ya Kombe la Dunia 1930, Ufaransa iliifunga Mexico mabao 4-1.

Pal Teleki, Hungary (1934)
Bao hili lilifungwa dakika ya 11 kwenye mechi ya ufunguzi wa fainali za 1934 kule Italia. Hungary iliichapa Misri mabao 4-2.

Pietro Ferraris, Italia (1938)
Fainali za mwaka 1938 zilizofanyika Ufaransa, Italia iliifunga Norway mabao 2-1 huku bao la kwanza likifungwa na Ferraris wa Kikosi cha Azzurri.

Ademir Menezes, Brazil (1950)
Wenyeji walifungua vyema fainali hizi baada ya kuichapa Mexico mabao 4-0 kwenye mechi ya ufunguzi. Bao la kwanza lilifungwa na Menezes katika dakika ya 30.

Oswaldo da Silva Baltazar, Brazil (1954)
Kwenye fainali za Kombe la Dunia 1954, Brazil ilipata nafasi ya kuifungua tena na Mexico na Wacheza Samba hao walizidi kuonyesha ubora wao wakishinda 5-0, huku bao la kwanza likifungwa na Baltazar katika dakika ya 23 ya mchezo.

Oreste Corbatta, Argentina (1958)
Corbata alihitaji dakika tatu tu baada ya filimbi ya kuanza mechi kufunga bao la kwanza la fainali za Kombe la Dunia 1958. Staa huyo wa Argentina alifunga bao hilo katika mechi dhidi ya Ujerumani Magharibi.

Francisco Zuluaga, Colombia (1962)
Utepe wa fainali za mwaka 1962 ulikatwa na Zuluaga wa Colombia kwa bao lake la dakika ya 19 kwa mkwaju wa penati.

Enrique Borja, Mexico (1966)
Baada ya mechi ya ufunguzi kuisha kwa sare ya 0-0, Borja alikata utepe kwa kufunga bao la kwanza la fainali hizi kwenye mechi kati ya Mexico na Ufaransa.

Wilfried Van Moer, Ubelgiji (1970)
Van Moer ndiye aliyefumania nyavu kwa mara ya kwanza katika fainali za Kombe la Dunia 1970 zilizofanyika huko Mexico. Van Moer alifunga bao hili dakika ya 12.

Paul Breitner, Ujerumani Magharibi (1974)
Breitner alifunga bao hili dakika ya 18 na kuiwezesha Ujerumani kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chile.

Bernard Lacombe, Ufaransa (1978)
Moja kati ya mabao ya mapema kwenye mechi za ufunguzi. Lacombe alifunga bao hili dakika ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya wenyeji Argentina.

Bruno Conti, Italia (1982)
Fainali za mwaka 1982 bao la kwanza lilifungwa na Conti wa Italia katika dakika ya 18.

Alessandro Altobelli, Italia (1986)
Altobelli alikata utepe wa fainali za mwaka 1986 zilizofanyika Mexico katika dakika ya 44.

Salvatore Schillaci, Italia (1990)
Italia iliendelea kukata utepe kwenye fainali za tatu mfululizo baada ya Schillaci kufunga bao la kwanza la fainali hizo.

Georges Bregy, Uswisi (1994)
Fainali za mwaka 1994 zilizofanyika Marekani zilifunguliwa rasmi kwa bao la Bregy wa Uswisi kunako dakika ya 39.

Cesar Sampaio, Brazil (1998)
Sampaio ndiyo alizizindua nyavu za fainali za mwaka 1998 kule Ufaransa baada ya kufunga bao la kwanza la fainali hizo katika dakika ya tano tu mchezo.

Papa Bouba Diop, Senegal (2002)
Hapa ilikuwa zamu ya Waafrika baada ya staa wa Senegal, Papa Bouba Diop kukata utepe wa fainali hizo katika dakika ya 30.

Philipp Lahm, Ujerumani (2006)
Fainali hizi zilifanyika Ujerumani na Wajerumani wenyewe ndiyo walikata utepe wa fainali hizi kwa bao la Philipp Lahm katika dakika ya 6.

Siphiwe Tshabalala, Afrika Kusini (2010)
Kama ilivyokuwa kwa Ujerumani, Afrika Kusini nao wakakata utepe wenyewe kwa bao la dakika ya 55 lililofungwa na Tshabalala.

Marcelo, Brazil (2014)
Mcheza kwao hutuza watu husema na hapo, staa mwingine wa nyumbani alikata utepe kwa kufunga bao kwenye fainali za Kombe la 2014 zilizofanyika Brazil. Marcelo ndiye aliyefunga bao la kwanza la fainali hizo katika dakika ya 11 tu ya mchezo.