#WC2018: Ndo ivyo tena

Muktasari:

  • Warembo kibao akiwamo mchumba wa Dele Alli, mrembo Ruby Mae, mkewe Jamie Vardy (Rebekah) na mademu wengine wa wanasoka hao Annabel Peyton, Megan Davison walikuwa matata huko jukwaani, wakati Kieran Trippier alipofunga kwa friikiki dakika ya tano tu ya mchezo.

MOSCOW, RUSSIA. KWA dakika 68 mademu wa England hawakushikika jukwaani wakiwashangilia ‘mabebi’ wao waliokuwa wakipambana uwanjani na kuongoza kwa bao 1-0 dhidi ya Croatia kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia iliyopigwa uwanjani Luzhniki juzi Jumatano usiku, kabla ya mambo kubadilika na wao kugeuka kuwa wafariji kwa mastaa hao baada ya filimbi ya mwisho.

Warembo kibao akiwamo mchumba wa Dele Alli, mrembo Ruby Mae, mkewe Jamie Vardy (Rebekah) na mademu wengine wa wanasoka hao Annabel Peyton, Megan Davison walikuwa matata huko jukwaani, wakati Kieran Trippier alipofunga kwa friikiki dakika ya tano tu ya mchezo.

Hadi mapumziko, England ilikuwa mbele kwa bao hilo na kila kitu kilionekana kama kitakuwa vizuri kabla ya Ivan Perisic kuja kutibua sherehe kwa kuisawazishia Croatia dakika ya 68.

Mechi hiyo ikaingia kwenye dakika 30 za ziada na hapo ndipo Mario Mandzukic, alipopiga chuma cha pili na kuwafanya wale mademu wa England waliokuwa na vurugu jukwaani, kuonekana mikono ikiwa kwenye mashavu na kuwa na shughuli nzito ya kuwatuliza wapendwa wao baada ya filimbi ya mwisho.

Hakukuwa na sherehe tena. Kipa Jordan Pickford alionekana kabisa akitaka kumwaga chozi mbele ya mrembo wake, Megan Davison. Kieran Tripper ilibidi tu apate kumbatio la faraja kutoka kwa mkewe, Charlotte. Harry Maguire alikuwa kwenye hali mbaya baada ya filimbi ya mwisho, lakini kipenzi chake, mrembo Fern Hawkins, alifanya kazi ya ziada kumfariji, wakati Jesse Lingard ilibidi tu apate faraja hiyo kutoka kwa mama yake mzazi, sawa na ilivyokuwa kwa Kyle Walker.

Hata Kocha Gareth Southgate alionekana kuwa na faraja baada ya kupata sapoti kutoka kwa mkewe, mrembo Alison baada ya filimbi ya mwisho, huku Ashley Young akipokea mabusu moto moto kutoka kwa mkewe Nicky Pike kabla ya kuonekana akiwa amembeba binti yake.

Ndiyo hivyo kilichowakuta England kwenye mechi yao dhidi ya Croatia na kuchapwa 2-1. Sasa wanasubiri kucheza mechi ya kuwania mshindi wa tatu dhidi ya Ubelgiji kesho Jumamosi.