Wema, Diamond kumbe ndo hivi!

Monday June 11 2018

 

By RHOBI CHACHA

BENDI kongwe ya muziki wa dansi, Mlimani Park ‘Sikinde’ waliwahi kuimba wimbo wa ‘Bubu Hutaka Kusema’ wenye mistari kadhaa ukiwamo huu; “Bubu hutaka kusema...ee mambo...mambo yanapomzidia...”

Wimbo huu uliotamba miaka ya 1980 unazungumza jinsi mtu asiyependa kusema anapozidiwa hushindwa kuvumilia na kusema.

Ndivyo, ilivyo kwa mlimbwende, Wema Sepetu ‘Madame’ aliyeamua kuvunja ukimya ikiwa ni siku chache tangu atue nchini kutoka India alipoenda kwenye matibabu. Wema ameamua kusema baada ya kutukanwa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya watu wasio wastaarabu.

Wema ameshambuliwa kwa lugha kali na za kejeli kwa kile kilichoelezwa kuwa, eti karudiana na staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz. Kutokana na kushindwa kuvumilia, mrembo na mwigizaji huyo amefunguka kwa kuwaambia wanamshambulia kuwa, wala wasisumbuke na kujipa tabu kumtusi. Wema anasema kuwa ameshayazoea matusi yao hata lile la kutokuzaa maana ndio tusi kubwa kwake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Miss Tanzania huyo wa mwaka 2006 anasema, watu hawajui jinsi anavyofurahia matusi yao katika mitandao ya kijamii tofauti na wenyewe wanavyodhani anachikuzwa nayo.

MSIKIENI MWENYEWE

Wema anasema matusi na kauli nyingine za ovyo ameshazoea kwani tangu amekuwa maarufu hadi sasa ameshatukanwa sana, kiasi kwamba awali alifikia hatua ya kukata tamaa ya kuishi dunia kwa tusi la kuambiwa mgumba.

Hata hivyo kwa kuamini kuwa Mungu ndiye mweza wa kila jambo na halimfiki mtu ila kwa mipango yake, ameamua kuwaachia wanaomtusi waendelee kujibebea dhambi.

“Hivi unajua watu wanajisumbua sana, pamoja na mimi kujieleza katika mitandao jinsi ninavyochukizwa na kashfa zao, wanashindwa kuelewa hisia zangu ziko wapi, hadi wamenisababisha nizoee matusi yao na kuyafurahia kwani hawana jipya.

“Kila siku mambo ni yale yale...mara mimi mgumba...mara sijui nabadilisha wanaume na matusi mengine ya nguoni kabisa ambayo wala hayanistui kwa sasa, nina imani ipo siku hata hili tusi la mgumba litakwisha kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, maana ndio tusi kubwa kwao kwa sasa,” anasema Mwema

VIPI ISHU YA DIAMOND

Wema wala hafichi kitu, anafungua ukweli ulivyo kwa kusema; “Sijarudiana na Diamond nilishasema hilo wazi, na ishu ya mimi kuitwa wifi na dada yake Esmah, mie naona alishazoea pindi niko na kaka’ake kimapenzi.”

“Ninachoshangaa watu wanaounganisha matukio kwa kuniambia mimi nimerudiana na Diamond. Watu wafahamu nina mchumba kwa sasa, tena anachukizwa na hizi habari zinazoongelewa katika mitandao juu yangu, kwani inafikia hatua mtu anadhani ni kweli niko na Diamond, wakati kwa sasa ni rafiki tu na kusaidiana katika kazi,” anasema.

Mwanadada huyo akawaomba wanaomsakama kuachana mara moja fikra kwamba amerejesha majeshi kwa Diamond, kwani watamvunjia uchumba wake kwa mpenzi wake wa sasa mwenye malengo naye ya maisha marefu.

KUTUMIKA WCB

Wema alipoulizwa imekuwaje amekuwa akitumika na Wasafi Classic iliyo chini ya Diamond na haoni kama ndio sababu ya kutupiwa makombora kwamba amerudiaha

majeshi kwa Chibu Dangote.

“Nasikia tu watu wanasema hivyo, ila naweza sema ni kweli natumika WCB, ila katika kazi huwa anapata malipo, tofauti na watu wanavyodhani kutumika kimapenzi au kiki zisizokuwa na faida, ndio maana niliwaambia Diamond nipo naye kikazi tu na sio ishu za mapenzi kwani kwa sasa ni zilipendwa. Watu waache na ushabiki wa mitandao hauna maana. Mitandao inapaswa kutumiwa kwa mambo ya maana, ” anasema Wema.

ISHU IPO HIVI

Wema anasema kipindi alipoachana na Diamond walikaa muda mrefu bila kupeana hata salamu, lakini baadaye walikaa chini na kumaliza tofauti zaona wakakubaliana wafanye kazi na kuyasahau masuala ya mapenzi.

Alipoulizwa kama aliwahi kujuta kuwa staa hasa baada ya kuwa Miss Tanzania kabla ya kutumbukia kwenye uigizaji filamu na Wema akafunguka;

“Yes, nimewahi kujuta lakini mwisho wa siku huwa nasema Mwenyezi Mungu ndiye mpangaji wa kila jambo, naamini yeye ndiye aliyenipangia kuwa hivi nilivyo leo. Kama asingetaka nisingefika hapa nilipo, hivyo kujuta kunatokea kwa kila mtu, lakini siwezi kukufuru.”

Mwanadada huyo amerejea nchini hivi karibuni kutoka India alipoenda kwa matibabu, licha ya kushindwa kuweka bayana kitu gani kilichokuwa kinamsumbua, licha ya kukiri ni mambo ya wanawake na amefanyiwa upasujai mdogo na kwa sasa yupo poa kabisa.