Unamkosaje Ferre Gola kwa mfano

Muktasari:

  • Onyesho hilo litakalofanyika mubashara Juni 29 kwenye Hoteli ya Serena na Julai Mosi katika ufukwe wa Escape one, Mikocheni, limeandaliwa na ubalozi wa DRC nchini na kudhaminiwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen, Clouds Media Group na Montage Limited.

MWANAMUZIKI raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ferre Gola atapagawisha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam katika onyesho la kuadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa DRC.

Onyesho hilo litakalofanyika mubashara Juni 29 kwenye Hoteli ya Serena na Julai Mosi katika ufukwe wa Escape one, Mikocheni, limeandaliwa na ubalozi wa DRC nchini na kudhaminiwa na Kampuni ya Mwananchi Communication Limited ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen, Clouds Media Group na Montage Limited.

Balozi wa DRC nchini, Jean Pierre Ntamba alisema; “Tunakusudia kuzichangia shule za kadhaa ikiwemo Uhuru maalumu, Wama Nakayama na Congo.”

Ferre Gola ni mwimbaji wa muziki wa rumba, mtunzi wa nyimbo na dansa, alizaliwa miaka 41 iliyopita katika Jiji la Kinshasa na alianza kutamba kwenye muziki na kundi la Bandalungwa kabla ya 1995 kujiunga na kundi la Wenge Musica.

1997-2004 alilitumikia kundi la Wenge Musica Maison Mere linaloongozwa na Werasson kabla ya kuanza kufanya shughuli zake binafsi za muziki 2006.

Miongoni mwa nyimbo ambazo mshindi huyo wa tuzo ya WatsUp TV Africa Music Video Awards mwaka 2016 ni Lubukulukumu unaozungumzia amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Albamu yake ya kwanza ya Sens Interdit ilivutia mashabiki wengi nchini Kongo na katika mataifa ya Uholanzi, Ubelgiji na Ufaransa.

Mwaka 2016 Ferre Gola alitajwa kuwa miongoni mwa wanamuziki 10 maarufu nchini DRC kwa mujibu wa mtandao wa mtandao wa Culturetrip.

Moja ya nyimbo zake zinazotamba ni ‘Tucheze’ alioimba na Victoria Kimani.