Mzimu wa mtoto staa huyu

Muktasari:

  • Mwigizaji huyo amefichua hilo akiwa kwenye maandalizi ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya kifo cha mwanaye, Raymond Ekwu shughuli itakayofanyika kwenye Kanisa la Redeemed Christian Church jijini Lagos.

KIFO cha mtoto wake wa kiume, bado kimeendelea kumpa maumivu makali mwigizaji, Eucharia Anunobi ambaye amedai atachukua muda mrefu kufuta kumbukumbu za pigo hilo alilolipata.

Mwigizaji huyo amefichua hilo akiwa kwenye maandalizi ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya kifo cha mwanaye, Raymond Ekwu shughuli itakayofanyika kwenye Kanisa la Redeemed Christian Church jijini Lagos.

“Sio jambo rahisi kukabiliana na jinamizi la kumpoteza mtoto wako pekee. Ni kovu ambalo litaendelea kuwepo. Nashindwa hata kujua kama nina nguvu. Watu wananiambia nina nguvu lakini najifahamu ni mwepesi na dhaifu.

“Nimesahau hata kupaka poda na lipstiki. Usiku na mchana nimekuwa kwenye kilio. Naendelea kukumbuka uwepo wake hasa ninapoendesha gari halafu nakumbuka hayupo tena. Alikuwa ananipa ukaribisho wa bashasha,” alisema kwa masikitiko, Anunobi.

Kifo cha mtoto huyo wa Anunobi kilitokea mwaka jana, kutokana na ugonjwa kansa ya damu ingawa yeye mwenyewe anadai kuwa kilitokana na uzembe wa madaktari.