Mwite Wema Isaac Sepetu a.k.a The drama Queen

Muktasari:

  • Wema ni binti wa Balozi Isaac Abraham Sepetu, aliyepata kutumikia nchi upande wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar katika nafasi ya uwaziri, akawa pia balozi wa Urusi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), vilevile alikuwa mbunge miongoni mwa wabunge wa mwanzoni kabisa katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

WEMA tena! Ndiyo pamoja na kizaazaa cha mbwa wa polisi kupotea na mkwara mzito uliochimbwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, lililobamba Ijumaa iliyopita ni hukumu ya kifungo cha mwaka mmoja jela au faini ya Sh2 milioni aliyohukumiwa Miss Tanzania 2006, Wema Isaac Sepetu.

Wema ni binti wa Balozi Isaac Abraham Sepetu, aliyepata kutumikia nchi upande wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar katika nafasi ya uwaziri, akawa pia balozi wa Urusi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), vilevile alikuwa mbunge miongoni mwa wabunge wa mwanzoni kabisa katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Balozi Sepetu alifariki dunia Oktoba 27, 2013. Hata hivyo, amewaachia Watanzania watoto tisa, akiwemo Wema. Hata alipokuwa hai, naye alipata kushuhudia vitimbi vya Wema. Leo ikiwa ni miaka mitano tangu kifo chake, Wema ni yuleyule, malkia wa tamthiliya zilizosheheni vitimbi, ukipenda unaweza kumwita The drama queen.

Hatia aliyokutwa nayo Wema katika hukumu aliyosomewa juzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni ya kutumia dawa za kulevya, vilevile kukutwa na dawa kulevya nyumbani kwake. Hivyo, kwa makosa hayo akahukumiwa ama kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini Sh2 milioni. Wema alilipa fedha hizo zote na sasa anadunda akiwa huru.

Februari 2, mwaka jana, Wema alikuwa miongoni mwa watu waliotajwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ama kwa kununua na kutumia au kufanya biashara moja kwa moja. Orodha hiyo ilitajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Wema alipekuliwa nyumbani kwake na kukutwa na misokoto ya bangi pamoja na karatasi ya kusokotea bangi, yaani rizla. Wema pia alipelekwa kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kupimwa mkojo kubaini kama anatumia dawa za kulevya au la! Hukumu imebainisha kuwa Wema alikutwa anatumia madude!

KESI IKAMPELEKA CHADEMA

Februari 23, mwaka jana, yaani siku 19 tangu alipotajwa kwenye orodha ya wauzaji na watumiaji wa unga, Wema alitinga Mahakama Kuu, kumuunga mkono Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Makonda kuhusu mamlaka yake ya kutuhumu watu kwenye kadamnasi na kuamuru wafike Polisi kwa mahojiano. Mbowe alitaka Mahakama itamke kuwa Makonda hana mamlaka hayo.

Vilevile Mbowe alitaka Mahakama itamke Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayowapa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya mamlaka ya kuamuru watu kuwekwa mahabusu kwa saa 48 imepitwa na wakati na inakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ikumbukwe Mbowe alikuwa mmoja wa waliotajwa na Makonda katika orodha ya Makonda ya wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya. Kwa msingi huo, Wema na Mbowe walikuwa na jambo lenye kufanana.

Kati ya busara zilizoachwa na mwanafalsafa wa Kanisa Katoliki, Mtakatifu Thomas Aquinas ni andiko la Kilatini kuhusu Nadharia ya Vita (Jus Bellum Iustum), kwa tafsiri ya Kiingereza ni Just War Theory. Nadharia hiyo ina pande mbili, kwanza ni Usahihi wa Kuingia Vitani (Jus Ad Bellum) na Usahihi wa Jinsi ya Kupigana Vita (Jus In Bello).

Wema alisimamia upande kuwa hakuwa akitumia wala kuuza dawa za kulevya. Hivyo, kipengele cha kwanza tayari Wema alishajiona anao usahihi wa kupigana vita, alionewa kutajwa na Makonda. Jinsi ya kupigana vita ni kupitia eneo la sheria. Alitaka kuuthibitishia umma wa Watanzania Makonda alimsingizia. Je, ubavu huo alikuwa nao?

Ni hapo Wema aliamua kuuchukua msemo kutoka kwenye lugha ya falsafa ya Kihindu, Jain, Buddha na Sikhi inayoitwa Sanskrit inayoeleza Adui wa Adui Yako ni Rafiki Yako (Enemy of Your Enemy is Your Friend).

Ukiwa na adui, halafu huyo adui yako akawa na adui mwingine, maana yake wewe na yule adui wa adui yako, mnakuwa mnachangia adui mmoja. Kwa vile adui yenu ni mmoja, basi mnatakiwa kuwa marafiki ili mshirikiane kupambana na adui yenu. Wema alitaka kuthibitisha Makonda alimsingizia. Hapohapo alimshuhudia Mbowe naye akipambana na Makonda. Ni hapo sasa Wema alijiunga na Mbowe kwa sababu walikuwa wanachangia adui, ambaye ni Makonda ili kupambana naye kisheria.

Mbowe ni Mwenyekiti wa Chadema na Chadema ina wanasheria, ni hapo Wema alipata mpaka wanasheria wa kumsimamia kesi yake dhidi ya Makonda. Kwa vile Chadema walikuwa mwanga wake katika mapambano yake dhidi ya Makonda, aliamua kuvaa gwanda kabisa.

Hivyo basi, Wema hakwenda Chadema kwa bahati mbaya, alikuwa kwenye harakati za kuunganisha jeshi dhidi ya Makonda. Alifanikiwa kwa Mbowe. Hata hivyo, yaliyofuata ni mwendelezo wa Wema kama The drama queen.

WEMA AKAREJEA CCM

Wema alipokuwa anahama CCM kujiunga na Chadema Februari mwaka jana, alisema kwa kile Kiingereza chake mithili ya mtu mwenye kupata shida ya kuzungumza Kiswahili kuwa anapofanya uamuzi ni jumla, huwa hageuki nyuma. Alisema: “There is no going back.”

Kuna aliyemwamini? Inawezekana Chadema walimwamini. Waliomjua Wema walisema “ngoja sasa tuone muvi”, maana Wema alidhalilishwa na Diamond Platnumz jukwaani Mlimani City mwaka 2012, alipokwenda kumtuza, lakini stadi huyo wa Bongo Fleva alimkaukia. Wema akasema Diamond ni mshamba na asingerudiana naye tena lakini walirudiana.

Mwaka 2013, Diamond alimrekodi Wema sauti akimbembeleza kimapenzi warudiane, kisha sauti hiyo akaivujisha mpaka kwenye vyombo vya habari. Wema akasema Diamond ana mambo ya Kiswahili, akaapa isingetokea tena yeye na Diamond kurudiana. Ikawaje? Wema alirudiana na Diamond. Kweli Wema alipokuwa Chadema ungedhani alimaanisha jinsi alivyokuwa kamanda. Mara Arusha na Godbless Lema, ungemwona jirani na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob. Alikuwa mbele kweli kwenye shughuli za ujenzi wa Chadema. Hata hivyo, Desemba Mosi, mwaka jana, Wema alitangaza kurejea CCM, akidai alipakumbuka nyumbani kwao, hakuwa na furaha ugenini.

Hivyo, drama za mapenzi yake na Diamond, akazipeleka mpaka kwenye siasa, akavigonganisha vyama viwili vikubwa nchini. Je, bado unaweza kubisha ukiambiwa kuwa Wema ni malkia wa drama?

Aliporejea CCM akapata wakili mpya. Alberto Msando ambaye ni mpinzani aliyerejea CCM akamsimamia kesi. Ungempitia kwenye akaunti yake ya Instagram, ungejionea namna ambavyo alivyokuwa anamimina sifa nyingi kwa Makonda. Akimwita “kaka, mpiganaji na kiongozi shupavu”.

Kumbuka Wema alisema huwa hageuki nyuma.

USHAURI KWA WEMA

Hukumu aliyopewa Wema yenye kumpa chaguo la kulipa faini ni nafuu kubwa kwake na hutakosea ukisema ni upendeleo mkubwa. Watu wengi wanakutwa na hatia ya mara moja wananyimwa kulipa faini na kuamriwa kwenda jela, ila yeye si mara ya kwanza bado kapewa fursa ya kulipa faini iliyo ndani ya uwezo wake.

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, aliachiwa kutoka jela Mei mwaka huu, alipokuwa akitumikia kifungo cha miezi mitano. Sugu alikutwa na hatia ya kuzungumza maneno yenye kumfedhehesha Rais. Katika hukumu yake hakupewa chaguo la faini ingawa lilikuwa kosa la kwanza. Ni jela tu.

Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali, Januari mwaka jana alikutwa na hatia ya kufanya vurugu kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, wakati wa uchaguzi wa baraza la madiwani. Lijualikali alihukumiwa kwenda jela miezi sita bila faini.

Hata hivyo, Lijualikali alishinda rufaa yake Mahakama Kuu baada ya kukaa jela miezi mitatu. Julai 23, 2008, fundi wa Bongo Fleva, Khalid Mohammed ‘TID’, alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, kwa kosa la kumjeruhi mtu katika ugomvi wa klabu akiwa amelewa. TID hakupewa fursa ya kulipa faini japokuwa lilikuwa kosa lake la kwanza.

Wema aliwahi kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kesi ikiwa kugombana na kuharibu gari la aliyekuwa boy friend wake, staa wa Bongo Movie, marehemu Steven Kanumba. Hata hivyo, kesi iliisha baada Kanumba kuomba kutoendelea na kesi.

Juni 9, 2011, Wema alihukumiwa kwenye Mahakama ya Mwanzo, Kinondoni, kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini Sh40,000 kwa kosa la kumtusi mwanamuziki na prodyuza wa Sharobaro Records, Raheem Nanji ‘Bob Junior’. Wema alilipa faini na kutakiwa na mahakama kutorudia tena kosa kama hilo.

Hivyo, Wema ni mzoefu wa matukio ya jinai, lakini ana bahati, kwani hajapewa adhabu ya jela moja kwa moja kama wengine wengi.

Hakimu wa juzi angeamua kuzingatia rekodi zake za nyuma, angeweza kumnyima fursa ya rufaa. Ni ushauri kwake kujichunga.

Tayari ana rekodi chafu na siku nyingine si rahisi kupewa dirisha la rufaa. Atatupwa jela. Si kila siku ni Ijumaa.