Masogange aisimamisha Mbeya

Sabri Shabani (mwenye kofia) na mwanawe Sania Sabri wakiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa mzazi mwenzake marehemu Agnes Gerald (Masogange). Mazishi ya msanii huyo yalifanyika nyumbani kwa wazazi wake Mbalinzi Wilaya ya Mbeya. Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

Msafara uliobeba mwili wa marehemu uliwasili nyumbani hapo saa 5:50 asubuhi ukiongozwa na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) maarufu kwa jina la Green Guard. Baada ya kuwasili, mwili huo uliingizwa kwenye nyumba ya baba yake mzazi, Gerald Waya, ambayo ilijengwa na Masogange.

SAFARI ya mwisho duniani ya aliyekuwa msanii maarufu nchini, Agnes Gerald ‘Masogange’ ilihitimishwa alasiri ya jana Jumatatu baada ya mwili wake kuzikwa nyumbani kwa wazazi wake, kijijini Utengule, Mbalizi, Mbeya.

Msafara uliobeba mwili wa marehemu uliwasili nyumbani hapo saa 5:50 asubuhi ukiongozwa na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) maarufu kwa jina la Green Guard. Baada ya kuwasili, mwili huo uliingizwa kwenye nyumba ya baba yake mzazi, Gerald Waya, ambayo ilijengwa na Masogange.

Mwili huo uliingizwa humo kwa ajili ya shughuli za kimila.

Baadhi ya wasanii waliosafiri kutoka Dar es Salaam ili kuhudhuria maziko hayo walianza kuwasili Mbeya alfajiri ya jana na kuendelea na shughuli nyingine za kimsiba nyumbani hapo.

Watu wazimia

Kitendo cha kufikishwa kwa jeneza la mwili wa marehemu Masogange, kilisababisha umati uliofurika msibani hapo kushindwa kujizuia, wengi wakiangusha vilio na wengine kupoteza fahamu kwa muda.

Wimbo wa Belle 9 ‘Masogange’ watumika

Wakati jeneza lenye mwili wa marehemu likiwa ndani, wimbo wa msanii Belle 9 wa ‘Masogange’ aliomshirikisha marehemu, ndio uliokuwa ukipigwa kuwafariji waombolezaji.

Wasanii kivutio

Mwili ukiwa bado ndani, shughuli nyingine nje zilisimama kwa takribani saa moja baada ya waombolezaji hususani vijana kuharibu taratibu kutokana na kila mmoja kutaka kupiga picha na wasanii maarufu waliokuwapo msibani hapo, jambo lililosababisha vurugu.

Ujio wa wasanii hao uligeuka neema kwa wengi wa waombolezaji hasa vijana waliojawa shauku ya kupiga nao picha.

Kutokana na vurugu hizo, waratibu wa shughuli za msibani hapo walilazimika kusitisha kwa muda shughuli ya kuutoa nje mwili wa marehemu kwa ajili ya ibada hadi walipofika askari na kudhibiti hali.

Baada ya mambo kutulia, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, waliwasili msibani hapo kwa ajili ya kuongoza mazishi hayo.

Akitoa salamu za rambirambi kutoka serikalini, Makalla, alisema hakuna mtu anayejiandaa wala aliye tayari kwa ajili ya kifo, hivyo kifo cha Masogange kitumike kutambua kwamba binadamu wote ni wasafiri hapa duniani.

“Nimefurahi namna wasanii mlivyojipanga bila kujali bifu na tofauti zenu, katika hili mmekuwa pamoja. Nimefuatilia tangu msiba ulipotokea, kwa mshikamano huu serikali tunawapongeza,” alisema.

“Pia niwapongeze wananchi kwa namna mlivyojitokeza kwa wingi na hii inaonesha ndio utamaduni wa Mtanzania kushirikiana katika matatizo.”

Akimshukuru Makalla kwa niaba ya wasanii wenzake, Mwenyekiti wa wasanii hao, Steve Nyerere, alisema: “Hili ni pigo kwetu wasanii na tumekubaliana kwamba sehemu ya kiasi tulichochanga kitatumika kulipia ada ya mwaka mmoja ya mtoto wa marehemu ambaye yupo darasa la saba, lakini pia kumlipia Bima ya Afya endelevu.”

Mdau kumsomesha mtoto

Mmiliki wa Shule ya Sekondari za St. Patrick za jijini Dar es Salaam Ndele Mwaselela, ametangaza kumsomesha bure mtoto wa marehemu Masogange, Sania Sabri, kuanzia Kidato cha Kwanza.

Alisema: “Na akifaulu Kidato cha Nne, pia nitamsomesha Kidato cha Tano na Sita, pia akifaulu hapo atakwenda Chuo Kikuu kwa gharama zangu.”

Belle 9 ashindwa kujizuia

Baada ya salamu za viongozi hao, msanii Belle 9 aliitwa jukwaani ili kuwaimbia waombolezaji wimbo Masogange, lakini alishindwa akiishia kuangusha kilio.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbeya, Akim Mwalupini, alisema sababu ya vijana wa chama chake kubeba jeneza la marehemu Masogange ni kwamba baba mzazi wa marehemu ni Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Utengule Usongwe.

Pia alisema Masogange alikuwa kada wa chama hicho hivyo iliwalazimu wahusike kwenye msiba huo. Masogange alifariki Ijumaa iliyopita akiwa katika Hospitali ya Mama Ngoma jijini Dar es Salaam.