Luizio ajiondoa Simba mapemaaa

WAKATI viongozi wa Simba wakisubiri ripoti ya kocha wao Pierre Lechantre kujua ni wachezaji gani atawapiga panga na anahitaji sura gani mpya, straika wa timu hiyo, Juma Luizio ameanza hesabu zake mapema.

Luizio aliliambia Mwanaspoti ana furaha kuona Simba imetwaa ubingwa na yeye amevaa medali, lakini anahitaji kukiokoa kipaji chake, huku akizipigia hesabu timu anazoziona zinaweza kumfaa kuwa ni Singida United, Lipuli, Mtibwa Sugar na Azam FC.

“Sitaki kwenda timu ili mradi tu, nahitaji kucheza na kupata ushindani wa kufanya nijitume, hizo timu nilizozitaja zinaonekana zina malengo katika Ligi Kuu.

“Nina malengo yangu, sioni fahari kukaa Simba wakati sichezi. Nadhani nitakuwa sikitendei haki kipaji changu, hivyo naona msimu ujao nitafanya uamuzi mwingine,” alisema.

Wakati Luizio ameona Lipuli ni moja ya timu anazoona zitamfaa, kocha wa timu hiyo Amri Said alisema wapo tayari kumpokea kwa mikono miwili kwa madai wao wanaona ni mchezaji mwenye madini mguuni.

“Sio kila mchezaji ambaye hapati nafasi Simba na Yanga, ukadhani kiwango chake kimekufa, Luizio bado ana madini mguuni na ni mchezaji ambaye namkubali, ana kasi ana nguvu naamini atakuwa msaada mkubwa.”