Irene utamu mwanzo mwisho

Tuesday September 12 2017

 

NYOTA wa filamu nchini, Irene Uwoya ametamba kuwa, kipaji alichonacho ni cha kipekee kwani licha ya kuwa zilipendwa, lakini bado hachuji akiendelea kukamua kana kwamba kaianza fani juzi tu.

Irene alisema kuthibitisha kuwa kipaji chake ni cha pekee ni jinsi alivyoingia kwenye fani na kunyakua tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike Chipukizi mwaka 2008 ya Vinara, lakini anaendelea kuwakimbiza wanaoibuka kwa sasa kwenye fani hiyo.

“Ubora wangu umedumu toka kuingia katika game kutokana na misimamo yangu katika kuangalia kazi za kucheza siigizii kila filamu, unajua mimi ndio muigizaji wa kike ambaye niliingia kwenye fani kwa kutwaa tuzo,” alisema Irene.

Irene alisema kutoshiriki sana kuigiza kila filamu kuna mfanya asipoteze umahiri wake na ubora wake katika kuigiza sinema zinazofanya vizuri, pia hapendi kuigiza filamu nyingi kwa mwaka.

Alisema kwa mwaka huu ameshiriki filamu moja tu ya Bei Kali na hajacheza kazi nyingine mpaka kwanza hiyo itoke.