Heh! Kumbe Riyama alikacha shule

Muktasari:

  • Riyama ambaye amekuwa kwenye filamu kwa zaidi ya miaka 10 sasa alisema kutokana na umbumbumbu wake alilazimika kuishia kidato cha pili baada ya masomo kuzidi kuwa magumu.

MWANADADA anayekimbiza kwenye tasnia ya filamu za Kibongo, Riyama Ally ameweka wazi kuwa hakumaliza elimu ya sekondari kutokana na ugumu wa masomo kwani hakuwa akiambulia chochote darasani licha ya walimu kujitahidi kufundisha kwa kiwango cha juu.

Riyama ambaye amekuwa kwenye filamu kwa zaidi ya miaka 10 sasa alisema kutokana na umbumbumbu wake alilazimika kuishia kidato cha pili baada ya masomo kuzidi kuwa magumu.

“Kwa kweli ugumu wa masomo ulinifanya niache shule, niliona kama wazazi wangu wanapoteza pesa yao bure, sikuwa naambulia chochote, walimu walikuwa wakijitahidi sana lakini sikuwa naelewa kitu, kwa hiyo nimekomea kidato cha pili, masomo ni magumu asikuambie mtu,” alisema Riyama.

Riyama ambaye ni bingwa wa kuigiza filamu za ushari na zenye kutia simanzi, alisema mbali na maeneo hayo mawili, anamudu pia kucheza vipengele mbalimbali vya filamu kwani ana kipaji kikubwa.